Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, amefanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba 851 zinazojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) huko Bunju B katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. 
 Waziri Magufuli ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Alhaj Eng. Mussa Iyombe, ametembelea eneo hilo ambalo tayari kuna nyumba 130 zinazoendelea kujengwa katika hatua mbali mbali. 
 Akionyesha kuridhishwa kwake, Waziri Magufuli ameipongeza TBA kwa ubunifu wao na jinsi ambavyo wanautekeleza mradi huo kwani nyumba zinazojengwa zimepangwa vizuri na ujenzi wake pia ukitekelezwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa. 
 Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo ambao ni sehemu ya ujenzi wa nyumba 10,000 ambazo TBA inatarajia kuzijenga nchi nzima kwa ajili ya kuwakopesha watumishi wa umma, Mtendaji Mkuu wa TBA Architect Elius Mwakalinga alielezea kuwa kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/14 jumla nyumba 2,500 zitajengwa katika mikoa 12 hapa nchini. Kati ya nyumba hizo mkoa wa Dar es Salaam utapata nyumba 1,400. 
 Hata hivyo, mbali na mafanikio hayo yaliyopatikana, changamoto kadhaa pia zimebainishwa ambazo zinahitaji kutafutiwa ufumbuzi ili kuweza kuutekeleza mradi huo kwa ufanisi. 
 Arch. Mwakalinga alibainisha kuwa mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ni moja ya changamoto kubwa walionayo kwa sasa. Alibainisha kuwa, baada ya kuwa na mazungumzo na taasisi mbali mbali za fedha, TBA iliwasilisha Wizara ya Ujenzi mapendekezo ya kuomba mikopo kutoka vyombo hivyo ambapo udhamini wa Hazina ulihitajika kabla ya kuendelea na taratibu nyingine. 
Mapendekezo hayo yaliyowasilishwa yamechukua muda mrefu kiasi cha kuathiri maendeleo ya mradi huo. Kutokana na hali hiyo TBA imelazimika kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuangalia utaratibu wa kuuza kupitia mikopo ya benki, nyumba 155 ambazo ziko katika hatua za mwisho wa ujenzi. Tayari TBA imeanza mazungumzo na benki za CRDB, Azania Bancorp, Barclays, ABC, TIB na NMB kwa ajili ya kuwapatia mikopo watumishi wenye sifa ambao wamekwisha wasilisha maombi ya kuziwa nyumba hizo. 
Jumla wa maombi 3,000 yamepokelewa TBA kutoka kwa watumishi wa ngazi mbali mbali. Nyumba hizo zinatarajiwa kuuzwa kwa kiasi cha kuanzia Shilingi milioni 30 hadi milioni 180 kulingana na ukubwa wa nyumba. 
 Katika hatua nyingine Waziri Magufuli ameidhinisha kutolewa kwa fedha kiasi cha Shilingi milioni 800 zilizopatikana kutokana na mauzo ya nyumba ambapo ameagiza kuwa taratibu zikamilishwe mara moja ili fedha hizo zitumike kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa Bunju B unaotekelezwa na TBA. 
Hadi sasa kiasi cha Shilingi bilioni 3.42 kimekwishatumika kwa ujenzi wa nyumba hizo pamoja na barabara zenye urefu wa kilometa 9.5 katika eneo hilo. 
 Waziri Magufuli hata hivyo imezitaka mamlaka zinazohusika na ujenzi na matengenezo ya barabara nchini ambazo ni TANROADS na Halmashauri mbali mbali kuhakikisha kuwa zinatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika maeneo ambayo yatajengwa nyumba zilizo katika miradi hii ya TBA kwani hilo ni jukumu lao na sio la TBA.
Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Elius Mwakalinga (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Magufuli (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Mussa Iyombe (kushoto) kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 851 zinazojengwa eneo la Bunju B jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Elius Mwakalinga (kushoto) akimwonyesha Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Magufuli (wa pili kulia) utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 851 zinazojengwa eneo la Bunju B jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Magufuli (mbele kulia) akikagua utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 851 zinazojengwa eneo la Bunju B jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Elius Mwakalinga.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Magufuli (katikati) akikagua utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 851 zinazojengwa eneo la Bunju B jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Mussa Iyombe (kulia) na Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Elius Mwakalinga (kushoto) pamoja na Watendaji wengine kutoka Wizara ya Ujenzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kila siku nyumba za watumishi wa umma sisi wa sekta binafsi mtatutafirije kama sio kutubagua ,Ningependa wajenge nyumba za wafanyakazi wapya (shart liwe waliograduate kuanzia mwaka 2005 kuja 2012)na sisi vijana wapya tununue nyumba,
    kwan uzoefu unaonyesha wenye nyumba ni wale wale wananunua nyingi na kujipatia faida na is wahitaji.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...