WAFANYAKAZI Wanawake wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa misaada kwa wagonjwa takriban 200 waliolazwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ya jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya wafanyakazi wa wanawake wa HESLB ndani ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Utafiti na kazi nyinginezo (RAAWU), Bi Octavia Selemani amesema kuwa wameafikiana kufanya hivyo kama taasisi ili kutoa mchango wao kwa wanajamii ambao wanahitaji zaidi msaada na faraja kutokana na kuwa katika hali ya maradhi sugu ya saratani.
Katika kutekeleza tukio hilo ambalo limefanyika wiki moja kabla ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, Wafanyakazi hao kutoka idara na vitengo mbalimbali vya taasisi hiyo ya serikali, wametoa msaada wa bidhaa za mahitaji ya kila siku ikiwa ni pamoja na mchele, unga wa sembe, maharage, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni za mche, sabuni za unga na dawa za meno.
Msaada huo wa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 2 ulikabidhiwa Jumamosi ya Machi mosi, 2014 kwa Muuguzi Mkuu wa zamu Bi Ofarasia Muhoha (Registered Nurse) kwa niaba ya uongozi wa taasisi hiyo.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 2014, Bi Octavia amesema kuwa siku hiyo wafanyakazi wanawake watashiriki shughuli za maadhimisho ikiwa ni pamoja na kuandamana na kusikiliza hotuba ya mgeni rasmi kupata ujumbe wa siku hiyo.
Baada ya maandamano, watakaa pamoja, kuzungumza na kutathmini mchango wao wa utendaji kazi katika kujenga taifa kwa kupima mafanikio dhidi ya changamoto wanazokabiliana nazo na kutafuta mbinu za kupata mafanikio zaidi.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya jitihada za wanawake katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa miaka iliyopita na kupanga mikakati ya mafanikio zaidi kwa miaka ijayo.
Katika baadhi ya nchi kama China, Russia, Vietnam na Bulgaria, siku hii ni ya mapumziko na inaadhimishwa kwa wananchi kuonyesha jinsi wanavyothamini na kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya nchi zao.
Mwaka huu maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kitaifa yanafanyika kwa ngazi ya mkoa yakiongozwa na kauli mbiu isemayo, “Chochea Mabadiliko kuleta Usawa wa Kijinsia”, ikisisitiza na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika kuandaa mipango, bajeti na programu za maendeleo katika jamii.
Jengo jipya la mawadi ya wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Mtaa wa Luthuli, Dar es Salaam.
Baadhi ya Wafanyakazi Wanawake wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wakishusha mahitaji kutoka kwenye gari tayari kuikabidhi wa uongozi wa ORCI.
Baadhi ya Wafanyakazi Wanawake wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wakijiandaa kuingia katika wodi la kwanza la wanaume ambako kuna wagonjwa 60.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...