Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Bw. Harbinder Signh Sethi (kushoto) na Katibu na Mwanasheria Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Joseph Makandege (wapili kushoto) wakikabidhi hundi ya shilingi milioni 11 kwa mwakilishi wa Kanisa la Mt. Rita Wakashia lililopo Kimara jijini Dar es Salaam, George Kashushura. Fedha hizo zitatumika kuanzisha SACCOS ya kanisa hilo, lenye lengo la kuwainua vijana kiuchumi. Makabidhiano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam jana
====== ======= =======
IPTL kusaidia miradi ya kuwawezesha vijana kiuchumi
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imeanza utekelezaji wa mpango wake wa kuiwezesha miradi mbali mbali inayowawezesha vijana wakitanzania kuimarika kiuchumi, ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya uchumi nchini.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 11 kwa kikundi cha kwaya cha kanisa la Mtakatifu Rita Wakashia lililopo Kimara jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Bw. Harbinder Singh Sethi alisema kampuni yake imejidhatiti katika kuhakikisa inatekeleza mipango yake ya kupiga jeki miradi ambayo itasaidia kuondoa umasikini na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini Tanzania.
“Hizi milioni 11 tulizotoa kwa Kanisa la Mt. Rita Wakashia, ambazo zitatumika katika uanzishwaji wa SACCOS kwa wanakwaya wa kanisa, ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wetu wa kuchangia katika kusaidia miradi ya kijamii na ya kiuchumi unaolenga kusaidia vijana wa kitanzania kuwa wachangiaji wakubwa katika ukuaji wa uchumi nchini,” alisema Singh.
Bw. Harbinder alisema mpango huo pia unalenga kusaidia mashule, makanisa, misikiti na makampuni mengine yasiyotengeneza faida yanayofanyakazi ili kuwawezesha vijana kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi Tanzania.
“Tunaamini kuwa SACCOS hii itakayoanzishwa itatoa fursa nzuri ya kujiwekea akiba nakutumika kama chanzo cha mikopo kwa vijana na wanakwaya wengine wa kanisa. Hii ni hatua kubwa katika kujikwamua kiuchumi katika jumuiya hii ya kanisa, ambayo ni taasisi isiyotengeneza faida,” alisema.
Naye Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL, Bw. Joseph Makandege alisema ili kuwapa sauti vijana na kuwaongezea fursa za kujiimarisha kiuchumi, IPTL kwa kushirikiana na kampuni ya Pan African Power (PAP) imetenga sehemu ya pato lake kwa ajili ya kupiga jeki miradi ya maendeleo ya kijamii, kwa dhamira ya kusaidia miradi ya kimaendeleo inayowalenga vijana.
“Sisi kama IPTL na PAP, tumeona kuwa ni jukumu letu kuisaidia jamii inayotuzunguka. Kwa kuanzisha SACCOS, ninaimani vijana wa kanisa la Mt. Rita Wakashia wataweza kuanzisha mradi madhubuti utakaowaletea mabadiliko chanya ya kiuchumi. Hii ndiyo sababu tulishawishika kutoa mtaji huu wa kuanzia ili kuwawezesha kuanzisha SACCOS,” alisema Bw. Makandege.
Akizungumza kwa niaba ya wanakwaya na waumini wengine wa kanisa hilo, Bw. George Kashushura alizishukuru IPTL na PAP kwa msaada wao na kubainisha kuwa fedha iliyotolewa itaelekezwa katika malengo mazuri yatakayobadilisha maisha ya vijana walio wengi.
“Fedha tulizopokea leo hii zitatumika kama mtaji wa kuanzisha SACCOS yetu ya kanisa ambayo itakuwa ni chachu ya mabadiliko ya maisha ya vijana walio wengi katika kanisa letu,” alisema Kashushura.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...