Na Mary Gwera. Mahakama ya Tanzania.
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imejipanga na imedhamiria kwa hali na mali kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa mlundikano wa kesi uliopo katika ngazi mbalimbali za Mahakama.
Aliyasema hayo alipokuwa akiongea na watumishi wa Mahakama mkoani Morogoro alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea Mahakama mkoani humo mwishoni mwa wiki.
“Hivi sasa takribani Majaji 55 wako katika mikoa mbalimbali nchini katika vikao vya kusikiliza mashauri (court sessions) lengo likiwa ni kumaliza mashauri ili kuondokana na Mashauri ya muda mrefu,” alisema Jaji Mkuu.
Aliongeza kuwa hivi sasa pia nguvu kubwa imewekwa katika kupata takwimu sahihi za Mashauri kutoka katika ngazi mbalimbali za Mahakama ili kujua ni mahali gani kuna mzigo mkubwa ili kuweza kuwekeza nguvu zaidi.
“Hivi sasa pia tumejikita katika kupata takwimu sahihi ili kuweza kujua ni mahali gani inabidi kuweka nguvu, zoezi la ukusanyaji takwimu tayari limekwishaanza kwa baadhi ya Maafisa wa Mahakama kusafiri ili kupata takwimu hizo, hivyo ninatoa rai kwa Wahusika kutuma taarifa/ takwimu zilizo sahihi ili kujua hali halisi,” alisisitiza.
Mhe. Jaji Mkuu alisema kuna mipango mingi ambayo Mahakama imejiwekea yote ikiwa imelenga katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao kwa wakati na kusema kuwa kwa sasa kila Jaji anapaswa kusikiliza na kumaliza jumla ya kesi 220 kwa mwaka.
“Tayari tumeshajiwekea kiwango cha kesi ambacho kila Jaji anapaswa kumaliza kwa mwaka ambacho ni kesi 220 kwa kila Jaji ndani ya mwaka, vilevile shauri linapoletwa Mahakamani linatakiwa kuwa limemalizika kwa kipindi kisichozidi miaka miwili (2),” alibainisha.
Alisema kuwa hivi sasa Mahakama ipo katika mchakato wa kuainisha idadi ya mashauri ambayo kila Hakimu anapaswa kusikiliza kwa mwaka, na kuongeza kuwa kwa sasa vituo vyote vitakavyobainika kuwa na mashauri mengi itabidi kuongeza nguvu kwa kuwatuma Mahakimu kutoka kituo kimoja kwenda kingine ili kusaidia kumaliza mashauri.
Mhe. Jaji Mkuu alisisitiza kuwa umalizwaji mashauri kwa wakati utategemea zaidi ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa Mahakama kwa kuwa na lengo moja ambalo ni kutochelewesha haki.
Kwa upande wake, Mhe. Hussein Kattanga Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, aliongelea juu ya maboresho ya Mahakama ambayo yanaendelea kwa sasa na kusema kuwa Mahakama kwa sasa imeweka kipaumbele katika kuwaendeleza Watumishi wake katika mafunzo mbalimbali. Alisema asilimia 6.2 ya bajeti ya mwaka huu imeelekezwa kwa ajili ya Mafunzo ya muda mfupi na mrefu na kuwataka watumishi wenye mahitaji ya kusoma kuomba nafasi za masomo ili waweze kupata ufadhili wa Mahakama.
Kwa upande wake, Mhe. Hussein Kattanga Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, aliongelea juu ya maboresho ya Mahakama ambayo yanaendelea kwa sasa na kusema kuwa Mahakama kwa sasa imeweka kipaumbele katika kuwaendeleza Watumishi wake katika mafunzo mbalimbali. Alisema asilimia 6.2 ya bajeti ya mwaka huu imeelekezwa kwa ajili ya Mafunzo ya muda mfupi na mrefu na kuwataka watumishi wenye mahitaji ya kusoma kuomba nafasi za masomo ili waweze kupata ufadhili wa Mahakama.
“Kwa sasa tunatengeneza mifumo mbalimbali ya kuweza kutatua matatizo ya watumishi wa Mahakama kwa pamoja na si kwa mtu mmoja mmoja, hali hii itawezesha kutatua changamoto nyingi zilizopo kwa wakati mmoja na hivyo kurahisisha utendaji kazi,” alisema Kattanga.
Miongoni mwa changamoto zilizoibuliwa katika Mahakama hizo ni uhaba wa vitendea kazi, uchakavu wa majengo, Uhaba wa watumishi katika baadhi ya Mahakama na mengineyo, hata hivyo uongozi wa Mahakama umeahidi kufanyia kazi changamoto hizo.
Katika ziara yake Mhe. Jaji Mkuu aliambatana na Mhe. Sekiet Kihio, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza, Naibu Msajili, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Pamoja na Mhe. Eddie Fussi, Kaimu Mkurugenzi wa Mahakama za Wilaya hadi Rufaa, Mhe. Euphemia Mingi, Mkurugenzi wa Mahakama za Mwanzo nchini na Bibi. Agatha Ng’ingo, Mkurugenzi Msaidizi- Rasilimali Watu.
Mhe. Jaji Mkuu na msafara alioambatana nao walipata nafasi kutembelea katika Mahakama ya Mkoa Morogoro, Mahakama ya Mwanzo Magole, Kiberege pamoja na Mahakama ya Wilaya –Ifakara- Kilombero.
Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Mohamed Othman akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe.
Joel Bendera alipofika ofisini kwake yeye pamoja na msafara ulioambatana nae
katika ziara ya kutembelea baadhi ya Mahakama zilizopo katika Mkoa huo.
Mhe. Mohamed Chande
Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania akisalimiana na Watumishi na pamoja na baadhi ya
wananchi wa Kijiji cha Magole Wilaya ya Kilosa alipofika kutembelea katika
Mahakama ya Mwanzo Magole iliyokumbwa na mafuriko hivi karibuni, aliye pembeni
ya Jaji Mkuu ni Mhe. Elias Tarimo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa. Uongozi wa Kijiji
cha Magole umetoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo kufuatia
kuharibiwa vibaya kwa mahakama iliyokuwepo. Mahakama nayo imeahidi kujenga
Mahakama ya Mwanzo katika kijiji hicho.
Mhe. Hussein
Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (kulia) akifafanua jambo mbele
ya Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania alipokuwa katika ofisi za
Mahakama ya Mkoa Morogoro, wanaosikiliza (wa pili kutoka kushoto ni), Mhe. Mary
Moyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mkoa Morogoro, wa pili kulia ni Bw.
Nestory Mujunangoma, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Morogoro.
Baadhi ya Watumishi
wa ngazi mbalimbali za Mahakama katika Mkoa wa Morogoro wakimsikiliza Mhe.
Mohamed Chande Othman alipokuwa akizungumza nao katika Mkutano aliofanya
alipofika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Miongoni mwa mabo
aliyoongoongelea Mhe. Jaji Mkuu ni pamoja na maboresho mbalimbali yanayoendelea
kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania lengo likiwa ni kuboresha maslahi ya
watumishi wake sambasamba na huduma ya utoaji haki nchini.
Baadhi ya Viongozi
walioambatana na Mhe. Jaji Mkuu katika ziara yake, wa kwanza kushoto ni Mhe.
Sekiet Kihio, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, (wa pili
kushoto) ni Mhe. Euphemia Mingi, Mkurugenzi wa Mahakama za Mwanzo Tanzania,
anayefuata ni Mhe. Eddie Fussi, Kaimu Mkurugenzi wa Mahakama za Wilaya hadi
Rufaa, anayefuata ni Bibi. Agatha Ng’ingo, Naibu Mkurugenzi Rasilimali Watu wa
Mahakama nyuma ni Mhe. Kevin Mhina, Naibu Katibu wa Jaji Mkuu.
1.
Mhe. Mohamed Chande
Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania, akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya
Ifakara Wilaya ya Kilombero alipotembele Mahakama hiyo katika kipindi cha ziara
yake aliyofanya mwishoni mwa wiki. (Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...