Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Bw. Andrii Deshchytsia akiwasilisha mbele ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Azimio ambalo pamoja na mambo mengine limeitaka Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika ya Kimataifa, kutoitambua kura ya maoni iliyopigwa March 16 ya kujitenga kwa Crimea kutoka Ukraine na hatimaye kujiunga na Urusi, Ukraine inasema kura hiyo ya maoni si halali na ni njama za kumega mipaka halali ya nchi yake. Azimio hilo lilipitishwa siku ya Alhamis kwa kura 100 za ndiyo, 11 za hapana na 58 hazikuegemea upande wowote.
Muwakilishi wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Balozi Vitaly I. Churkin akitoa maelezo kuhusiana na Azimio hilo lilowasilishwa na Ukraine na kuungwa mkono na nchi nyingi za Magharibi na zile za Ulaya, kwamba, kujitenga kwa Crimea kulikuwa halali na Urusi haikuwa na namna nyingine bali kuitambua kura hiyo na kusisitiza kwamba kihistoria Crimea ni sehemu ya Urusi.

Na Mwandishi Maalum

Wakati hali ya sintofahamu ikiendelea kuwa tete kufuatia Crimea kuamua kupiga kura ya maoni na hivyo kujitenga kutoka Ukraine na kasha kujiunga na Urusi.Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jana alhamisi, limepiga kura kupitisha na kuunga mkono azimio ambalo pamoja na mambo mengine, linaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuto tambua kwa namna yoyote iile kura hiyo na kujitenga kwa Crimea kutoka Ukraine.

Kabla ya tukio la upigaji kura kufanyika, baadhi ya wajumbe wanaoziwakilisha nchi zao, walitoa maelezo ya kwa nini nchi zao zilikuwa zimeamua kupiga kura ya ama kuunga mkono azimio , kutoliunga mkono au kutoegemea upande wowote. Baada ya maelezo hayo, matokeo ya kura yalikuwa ifuatavyo, Nchi 100 zilipiga kura ya ndiyo, nchi 11 zikipiga kura ya kulikataa azimio wakati nchi 58 zenyewe ziliamua kupiga kura ya kutoegemea upande wowote.

Azimio hilo liliwasilishwa mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na Bw. Andrii Deschcytsia, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine ambaye katika uwasilishaji wake alijenga hoja zilizowataka wajumbe kuliunga mkono azimio hilo.

Naye Muwakilishi wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Balozi Vitaly I.

Churkin yeye pamoja na kutetea uamuzi wa serikali yake wa siyo tu kutambua kura hiyo ya maoni lakini pia kujitenga kwa Crimea, alitoa hoja ya kutaka upigaji wa kura hiyo uwe ni wa kura zilizohesabiwa ( recorded vote).

Balozi Churkin alisititiza kwamba, kura ya maoni iliyopigwa na wananchi wa Crimea na hatimaye kuamua kujitenga na kisha kujiunga na Urusi ilikuwa ni ni kura halali na kwamba Urusi haikuwa na namna nyingine zaidi ya kuitambua kura hiyo.

Aidha kupitia azimio hilo ambalo limepitishwa baada ya Baraza Kuu la Usalama kushindwa kupitisha azimio kama hilo mnamo March 15 siku moja kabla ya kura ya maoni kufanyika baada ya Urusi kulipinga, linayataka pia Mashirika ya Kimataifa kuto tambua kujitenga kwa Crimea na jiji la Sevastopol kwa mujibu wa kura ya maoni ya March 16.

Ingawa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio hilo, azimio linakosa nguvu kama ambavyo lingepitishwa na Baraza Kuu la Usalama.

Wengi wa wazungumzaji waliounga mkono azimio hilo, au hata wale ambao hawakuegemea upande wowote,wamesisitiza haja na umuhimu wa kuheshimu Katiba ya Umoja wa Mataifa pamoja na Misingi ya sheria za kimataifa, ambazo pamoja na mambo mengine zinasisitiza kuheshimiwa kwa mipaka ya nchi na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyigine, pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano.

Baadhi ya wazungumzaji, wameleezea wasiwasi wao kuhusu kupitishwa wa azimio hilo ambalo limeungwa mkono karibu na nchi zote za Magharibi na zile za Ulaya kuwa kwa kufanya hivyo ni sawa na kuchochea zaidi mgogoro huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. wamarekani wamepata mtemi wao mara hii, wao wamezoea kuingilia nchi za watu ziko maelfu ya maili mbali na nchi yao kama iraki na afaganistani , sasa huyu nendeni mkapigane nae kama mna ubavu , mmebakia kuweka vikwazo vya uchumi , wakati mrusi huyo huyo mnamtumia akupelekeeni wanaanga wenu juu. Ubavu wa marekani kuonea nchi za kinyonge tu , mjaribuni basi na mrusi tuone nani mbabe ili tujue

    ReplyDelete
  2. Kutokana na siasa za kimataifa za siku hizi inabidi ile Jumuia Ya Nchi Zisizofungamanga na Upande wowote(Non-Aligned Nations) ifufuliwe.

    Mdau
    Christos Papachristou
    Diaspoara

    ReplyDelete
  3. Ndugu yangu wa kwanza hapo juu, jua hamna nchi yenye ubavu wa kum piga mmarekani kivita just so u know. Russia they are not as powerful as they being portrayed to be! Get it right ndugu yangu! What happen in Crimea is not a threat to the world like what it was in Afghanistan na Iraq na hamna ukiukwaji wa haki za binadamu na uteswaji wa watu, Russia wamevuka mpaka tuu. That's the issue Kama umefuatilia sana au hata kidogo ungejua haya. Mdau Tabata.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...