Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe akiendesha kikao cha 43 cha chombo hicho cha utendaji cha Jumuiya ya Madola Jijini London Uingereza.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi 9 zinazounda Kikosi Kazi cha Jumuiya ya Madola chini ya Uenyekiti wa Tanzania wakishiriki kwenye Mazungumzo na waandishi wa Habari baada ya kumaliza kikao chake cha 43 jijini London Uingereza.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi 9 zinazounda Kikosi Kazi cha Jumuiya ya Madola chini ya Uenyekiti wa Tanzania wakishiriki kwenye Mazungumzo na waandishi wa Habari baada ya kumaliza kikao chake cha 43 jijini London Uingereza.
Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania akiwa kwenye kikao na Mabalozi wa Nchi za Afrika Wanachama wa Jumuiya ya Madola jijini London, pembezoni mwa kikao cha Mawaziri wa Kikosi Kazi cha Jumuiya hiyo.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mhe. Peter Kallaghe akimkaribisha Mhe. Bernard Membe, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Madola kuzungumza na Mabalozi wa Nchi za Kiafrika wanachama wa Jumuiya hiyo.
----------------------------------------
Kikao cha 43 cha Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Jumuiya ya Madola kimeipunguzia adhabu nchi ya Fiji na hivyo kuiruhusu kushiriki kwenye baadhi ya matukio ikiwemo michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka 2014.
Kikao hicho kilichofanyika Jijini London Uingereza chini ya uenyekiti wa Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kilifikia uamuzi huo baada ya kupitia na kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Fiji katika kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao ikiwa ni jitihada za kutetea uanachama wake ndani ya jumuiya hiyo.
Akiongoza mjadala huo, Mhe. Membe alisifu hatua za makusudi zilizochukuliwa na nchi hiyo kama vile kushugulikia masuala ya haki za binadamu na utawala bora, kuanzisha daftari la kudumu la wapigakura, kuandaa mazingira ya uwazi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Septemba 2014 ikiwemo kuandaa mazungumzo na wadau mbalimbali wa siasa na aliyekuwaWaziri Mkuu aliyeingia kijeshi kujiuzulu na kugombea kama raia.
Akiendesha kikao hicho cha kwanza kama mwenyekiti wa chombo hicho muhimu, Mhe. Membe alisisitiza umuhimu wa kikosi kazi hicho kutekeleza majukumu yake bila urasimu na ubaguzi bali kwa kutoa fursa sawa za ushiriki wa nchi wanachama na kuzingatia misingi ya haki kwa manufaa ya wanachama wote.
Mhe. Membe pia aliwasisitizia mawaziri wenzake wanao tumikia chombo hicho kuwa makini na kuheshimu mila na desturi za nchi wanachama hususan zile za Kiafrika na kuepuka kushinikiza ajenda ambazo zinagusa dini, tamaduni na mila za nchi nyingi za kiafrika, kama vile ndoa za jinsia moja. Alisema kwa kufanya hivyo Jumuiya ya Madola itahatarisha muungano na mshikamano uliopo sasa ndani ya jumuiya hiyo.
Aidha, Mhe. Membe alisema hazina kubwa ya Jumuiya ni wingi wa nchi wanachama na tamaduni na desturi mbalimbali zinazowakilishwa na wanajumuiya. Hivyo kuheshimu tamaduni zote ndio kutajenga heshima ya Jumuiya ya Madola kimataifa.
Akiwashukuru wajumbe wa kikosi kazi kama mwenyekiti, Mhe. Membe alisema jukumu la uenyekiti wa chombo hicho si dogo, lakini wajumbe wa chombo hicho wakiungana kwa pamoja na kwa msaada wa Sekretarieti yaJumuiyayaMadolaanahakikandaniyamiakamiwiliyauenyekiti wake Jumuiya hiyo itaendelea kusimamia misingi muhimu ya jumuiya hiyo bila kutetereka.
Mhe. Membe ameiwakilisha Tanzania kama Waziri mwenye dhamana kuanzia mwaka 2011 akiwa kama mjumbe, na mwaka 2013 Jijini Colombo Sri Lanka alichaguliwa bila kupingwa kuwa mwenyekiti kwa miaka miwili. Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Mhe. Murray McCully alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.
Ukiacha Tanzania na New Zealand, wajumbe wengine ni mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi saba ambazo ni Cyprus, Guyana, India, Pakistan, Sierra Leone, Visiwa vya Solomon na Sri Lanka ambao wanaingia kwa nafasi yao ya uenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
18 Machi, 2014
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...