Mkuu wa wilaya ya Makete mh. Josephine Matiro (kushoto) akimkabidhi bati Bi. Ami Mahenge, ambaye ni mmoja kati ya waathirika wa kimbunga katika kijiji cha Ndulamo, Makete. 
 Mkuu wa wilaya ya Makete Mh Josephine Matiro akiwa na waathirika hao muda mchache kabla ya kuwakabidhi.
 Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akizungumza na waathirika wa kimbunga katika ofisi za kijiji cha Ndulamo.
 Kaimu mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Peter Mwagilo akizungumza na waathirika wa kimbunga (hawapo pichani) wakati wa kuwakabidhi bati kama walivyoahidiwa na serikali.
 Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akizungumza kabla ya kukabidhi bati kwa waathirika wa kimbunga katika kijiji cha Ndulamo.
 Bati zenyewe.Picha zote na habari na Edwin Moshi.
=====
Kufuatia maafa yaliyokikumba kijiji cha Ndulamo wilayani Makete mkoa wa Njombe ya nyumba 10 kuezuliwa na kimbunga mwishoni mwa mwezi februari mwaka huu, halmashauri ya wilaya ya Makete kwa kushirikiana na mfuko wa jimbo, hii leo wamekabidhi bati 180 kwa waathirika wa maafa hayo.
Akizungumza na waathirika wa tukio hilo wakati wa kukabidhi bati hizo zenye thamani ya tsh. milioni 2.5, mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro amesema kufuatia mkutano uliofanyika baina ya serikali na wananchi wa kijiji hicho, waligawana majukumu ambapo serikali iliahidi kutoa bati kwa wananchi hao, na hii leo imetekelezwa.
Mh. Matiro amesema ingawa msaada huo haukuwa asilimia 100 kwa waathirika wote lakini wamepatiwa zaidi ya robo tatu hivyo kiasi kilichobakia ni kidogo na kuwaomba wananchi hao kumalizia gharama zilizobaki.
"Mfano mtu alikuwa ameharibikiwa nyumba yenye bati 24, hapa serikali inampa bati 20 na hizo nne anatakiwa azigharamie yeye mwenyewe, na hii ni kutokana na msaada huo kuhitajika katika vijiji vingine viwili vya makete ambavyo vilikumbwa na maafa tena ili kila mmoja apate kidogo kidogo" amesema Matiro.

Amesema kwa hivi sasa hawana budi pia kumshukuru mbunge wa jimbo la Makete ambaye pia ni waziri wa mazingira Dkt. Binilith Mahenge kwa jitihada zake na uongozi wa wilaya kwa ujumla kuhakikisha wananchi hao wanapata bati hizo na kuwaomba wananchi hao kuzitumia kwa makusudi yaliyopangwa na si kuziuza.
Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya, kaimu mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Peter Mwagilo amesema ilifanyika tahmini ya kina na wataalamu wa halmashauri mara baada ya maafa hayo kuwakumba wananchi hao, na hivyo kila mwananchi atapewa bati kulingana na ukubwa wa tatizo lake.
"Kwa mfano wapo waliopata maafa kidogo wanahitaji bati chache, wengine bati mbili hao watapata zote mbili, lakini wale waliopata maafa makubwa watapata bati nyingi ila kila mmoja atagharamia kiasi kidogo pale palipopelea" alisema kaimu mkurugenzi.
Naye mmoja wa waathirika hao akizungumza na mwandishi wetu baada ya kukabidhiwa bati zake Bi. Ami Mahenge amesema anaishukuru serikali kwa msaada huo aliopewa na kuongeza kuwa kutokana na maafa hayo yaliyomkumba hakujua hatima ya maisha yake, ukizingatia yeye kukosa uwezo wa kifedha lakini msaada huo umekuwa mkombozi wa maisha yake.
Bi. Mahenge ametoa wito kwa waathirika wenzake kuhakikisha wanatumia ipasavyo msaada huo, kwa kuwa kumekuwa na kasumba ya kutumia vibaya misaada na baadaye wanaishia kulalamika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...