Na Mwandishi Maalum 
Wajumbe wanaohudhuria Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, wamepewa changamoto ya kuhakikisha kwamba, Takwimu rasmi na sahihi zinaunga mkono pamoja na mambo mengine, utekelezaji na usimamizi wa Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu ( SDGs) baada ya 2015. 
Changamoto hiyo imetolewa siku ya Jumanne na Katibu Mkuu Msaidizi Bw. WU HONGBO anayeongoza Baraza la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC). Bw. HONGBO alikuwa akifungua rasmi mkutano wa wiki moja wa wajumbe wanaounda Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa. 
Wajumbe hao ni kutoka nchi 24 ikiwamo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ujumbe wake katika Mkutano huu unaongozwa na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Idara Kuu ya Taifa ya Takwimu. Bw. WU HONGBO amewaeleza wataalamu hao wa masuala ya Takwimu kwamba, mwezi wa Tisa mwaka huu, Umoja wa Mataifa, utaandaa mikutano kadhaa ya kilele, ukiwamo Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu maendeleo ya mataifa ya visiwa vidogo. 
Ni katika kipindi hicho hicho pia ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaalika Wakuu wa Nchi na Serikali, wafanyabiashara, vyama visivyo ya kiserikali, na watu wa kada mbalimbali kuhudhuria mkutano wa kilele kuhusua masuala ya mabadiliko ya Tabia nchi. 
“ Hivi sasa kuna mchakato unaoendelea wa majadiliano ya wazi ya Kikundi Kazi kuhusu ajenda mpya za Malengo ya Maendeleo Endelevu baada ya 2015 ( SDGs). Majadiliano haya na mengine , ni wazi kwamba nafasi na mchango wa Takwimu ni muhimu sana katika kuchangia na kutoa mwongozo wa uundaji wa será na uundwaji wa kamati za ufuatiliaji wa utekeleazaji wa makubaliano yatakayofikiwa” akasisitiza Katibu Mkuu Msaidizi Katika kuhakikisha kwamba, wataalamu hao kutoka Taasisi za Kitaifa za Takwimu wanafuatilia kwa karibu mikutano mbalimbali muhimu inayoendelea katika Umoja wa Mataifa, yakiwamo majadiliano ya Kikosi Kazi kuhusu Maendeleo Endelevu baada ya 2015. 
Katibu Mkuu Msaidizi, Bw. HONGBO amesema, wakati mkutano huo wa Kamishieni ya Takwimu ukifanyika, katika ukumbi mwingine, kulikuwa kukiendelea majadiliano ya awamu ya tisa kuhusu maendeleo endelevu baada ya 2015. 
“ Wiki hii inatoa fursa ya aina yake kwenu, pamoja na ajenda mbalimbali zinazowakutanisha hapa, na wakati huu mkiendelea na mkutano wenu, kuna mkutano unaoendelea kuhusu maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo. Itakuwa vema na ni matumaini yangu kuwa mtaitumia fursa hii kuwasiliana na kubadilishana mawazo na wajumbe wenzenu wanaohudhuria mkutano huo. Lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba malengo hayo mapya ya maendeleo endelevu utekelezaji wake unaungwa mkono na Takwimu rasmi na endelevu” akasisitiza. 
 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi 30 ambazo ziliteuliwa kushiriki katika majadiliano ya Kikosi Kazi kuhusu maandalizi hayo ya SGDs baada ya 2015. 
Katika mzunguko huu wa tisa wa majadiliano wa hayo kuhusu SDGs, Tanzania inawakilishwa na Dkt. Lorah Madete, Afisa Mkuu na mchambuzi wa Sera kutoka Ofisi ya Rais, Kamisheni ya Mipango.
Mkurugenzi Mkuu, Idara Kuu ya Taifa ya  Takwimu Dkt. Albina Chuwa anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya  Takwimu ya Umoja wa Mataifa,  akifuatilia kwa makini hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo wa wiki moja Unaofanyika   hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi 24  ambazo ni Wajumbe wa  Kamisheni hiyo. Mkutano wa Kamisheni  ulifunguliwa na  Bw. WU HONGBO, Katibu Mkuu Msaidizi  anayeongoza Baraza la Umoja wa Mataifa la Uchumi na  Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC)   Katika Hotuba yake  Bw. HONGBO ametoa changamoto kwa wataalamu hao wa Takwimu  ya kuhakikisha kwamba wanafuatilia kwa karibu  majadiliano yanayoendelea kuhusu ajenda mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015 kwa kile alichosema, utekelezaji wa malengo hayo  utahitaji kuungwa mkono na takwimu rasmi na endelevu.  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...