
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Prof. John Nkoma akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa ushirikiano wa mtandao wa ATM za Umoja na M-pesa unaowawezesha wateja wa M-pesa kutoa fedha kupitia ATM za mtandao huo nchi nzima. Kulia ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Kelvin Tiwssa na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Switch Danstan Mbilinyi. Hafla hiyo imefanyika jijini Dar es salaam. Huo ni ushirikiano wa kwanza unaohuisha mtandao wa ATM za benki zaidi ya 20 na huduma za kifedha za simu ya mkononi.
Kutoka kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Switch Dunstan Mbilinyi, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Prof. John Nkoma na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Kampuni ya Vodacom Tanzania Kelvin Twissa (wa kwanza kulia) wakifurahia Mkuu wa Masoko wa M-pesa Isaac Nchunda kufanikiwa kutoa fedha kwenye M-pesa kupitia ATM ya Umoja ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kuzinduliwa kwa huduma inayowawezesha wateja wa M-pesa kutoa fedha kupitia ATM hizo nchi nzima. Huo ni ushirikiano wa kwanza unaohusisha mtandao wa ATM za benki zaidi ya 20 na huduma za kifedha za simu ya mkononi.
Mkuu wa Masoko wa M-pesa Isaac Nchunda (wa pili kulia) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi huduma mpya ya utoaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya M-pesa kupitia ATM za Umoja inavyofanyakazi muda mfupi baada ya uzinduzi rasmi wa huduma hiyo. Wanaoonekana pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Prof. John Nkoma (wa pili kushoto), Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Kelvin Twissa(wa kwanza kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Switch Danstan Mbilinyi.
Mkuu wa Masoko wa M-pesa Isaac Nchunda (wa pili kulia) akifanya muamala
wa kutoa fedha kutoka M-pesa kupitia ATM ya Umoja muda mfupi baada ya
huduma hiyo kuzinduliwa rasmi jijini Dar es salaam. Wanaoshuhudia tukio
hilo la kihistoria ni Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Prof.John Nkoma (wa pili
kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Switch Danstan Mbilinyi (wa
kwanza kushoto) na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Kelvin
Twissa.Huo ni ushirikiano wa kwanza unaohuisha mtandao wa ATM za benki
zaidi ya 20 na huduma za kifedha za simu ya mkononi
======= ====== ======
TCRA yapongeza Ushirikiano wa Vodacom na UmojaSwitch
* Ni baada ya Kuunganishwa kwa huduma ya M pesa na ATM za UmojaSwitch.
* Ni baada ya Kuunganishwa kwa huduma ya M pesa na ATM za UmojaSwitch.
* Wateja wa M pesa sasa kutoa fedha katika ATM za UmojaSwitch
Dar es Salaam, Machi 19, 2014 ... Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,(TCRA) imesema inafurahishwa na ukuaji na maendeleo ya kasi ya teknolojia ya simu za mkononi katika kuboresha maisha ya watu na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Prof. John Nkoma wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ushrikiano kati ya Kampuni ya Umoja Switch na Vodacom Tanzania kupitia huduma yake ya M-pesa utakao wawezesha wateja wa Mpesa kutoa fedha kupitia ATM za mtandao wa Umoja nchi nzima.
M-pesa ndio huduma inayoongoza miongoni mwa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi ikiwa na mtandao mpana zaidi wa mawakala zaidi ya 65,000 walioenea nchi nzima na hivyo kuiwezesha huduma hiyo kuwa rahisi zaidi kupatikana.
Prof. John Nkoma amepongeza ushirikiano huo katika kile alichokiita kuwa kitaendeleza mafanikio ya ukuaji wa tekonolojia ya simu za mkononi ikiwemo M-pesa huku akitanabaisha kuwa mamlaka yake imekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinarahisisha maisha ya Watanzania kwa kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku iwe katika kilimo na ufugaji, biashara na hata katika masuala ya kifamilia.
"Sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano tumefurahishwa sana kwa ushirikiano huu, katika utoaji wa Leseni tunazo za aina nne moja ya miundombinu, huduma, matumizi na utangazaji. Katika Leseni ya Miundombinu huu ni mfano vizuri wa kutumia teknolojia ambapo sekta ya fedha zinaungana na sekta ya Mawasiliano katika kutoa huduma kwa Watanzania." Alisema Prof. Nkoma na kuongeza.
"Uwepo wa huduma hii utawawezesha Watanzania wengi kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi, haya ni maendeleo mazuri sana katika sekta ya Mawasiliano na sekta ya fedha, sasa hizi wananchi wanaweza kuchukua huduma nyingi sana, hili sio jambo dogo hivyo kwa namna ya upekee kabisa ningependa kuwapongeza Vodacom na Umoja Switch kwa kuwezesha Ushirikiano huu."
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa, alibainisha kwamba wateja sasa wanaweza wakatumia mashine za ATM za Umoja Switch sehemu yoyote ya nchi kufanya miamala yao ya kifedha.
"M Pesa imepiga hatua nyingine ya juu zaidi. Wateja wetu sasa hawana wasi wasi tena kwani wanaweza kutoa fedha kutoka katika Akaunti zao za M pesa kupitia ATM za UmojaSwitch mahali popote."
"Hii ni hatua kubwa tumepiga kwetu sisi wote na tutaendelea kuwaletea huduma na bidhaa nyingi zaidi sokoni," alisema Twissa na kuongezea kwamba, "M Pesa inaendelea kubadilika kulingana na maendeleo ya kiteknolojia ambayo yamelenga kuihudumia wateja wetu vizuri zaidi."
Mtandao wa Umojaswitch umeanzishwa mwaka 2006 ukiunganisha benki zaidi ya 24 nchini na ATM takribani 200. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UmojaSwitch Bw.Danford Mbilinyi amesema kuwa anashukuru sana ushirikiano huu na Vodacom na kubainisha kwamba hii itasaidia katika kuwahudumia wateja ipasavyo mahali popote walipo.
"Hii ni siku kubwa sio tu kwetu sisi bali hata kwa wateja wetu pia. Ushirikiano huu ni wa aina yake kwetu sisi, na tunawashukuru sana Vodacom kwa kuamua kuja kwetu sisi." Alisema Mbilinyi.
Mpaka sasa huduma ya M Pesa inayotolewa na Vodacom inajivunia kuwa na mawakala takribani 65,000 waliosambaa nchi nzima, ambao siku zote wapo tayari kuwahudumia wateja wetu.
Huduma hii pia imekuwa ikiingia katika ushirikiano na mabenki na makampuni mengine nchini, wateja wetu sasa wana uwezo wa kununua bidhaa na huduma mbali mbali na kufanya malipo kupitia M Pesa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...