Na Saidi Mkabakuli 
Maendeleo ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu kufuatia kuendelea vyema kasi ya kundaza bomba hilo. 
Wakizungumza na wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Wahandisi wa Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita Yagela na Mhandisi Omary Kitiku wamesema kuwa kasi ya sasa ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo kijiji cha Madimba, mkoani Mtwara inatia moyo na hivyo kuashiria kukamilika kwa mchakato huo kwa wakati. 
“Mpaka sasa jumla ya kilomita 350 kati ya kilomita 492 za bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zimeshatandazwa hali inayokwenda sambamba na mpangokazi wa ujenzi wa kiwanda hiki,” alisema Mhandisi Yagela. 
Kwa mujibu wa Mpangokazi wa ujenzi wa kiwanda hiko hadi kufikia mwisho wa Julai kiwanda kinatakiwa kukamilika, na mpaka sasa, makazi ya wafanyakazi imekamilika. 
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mmoja wa viongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alisema kwamba kukamilika kwa bomba hilo kunatoa mwanya wa kukamilika kwa wakati uzalishaji wa umeme katika vituo vya Kinyerezi, jijini Dar es Salaam. 
“Kukamilika kwa bomba hili kunatoa fursa ya kwa Mradi wa kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 150 na Megawati 240 kwa kutumia gesi asilia vilivyopo Kinyerezi, jijini Dar es Salaam,” alisema Bibi Mwanri. 
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16), Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya nishati ambapo nguvu kubwa imewekwa katika uwekezaji wa miundombinu ya nishati ambapo utekelezaji wa ujenzi wa bomba la gesi Mtwara hadi Dar es Salaam unafanywa sambamba na ujenzi wa mitambo miwili ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi katika eneo la Kinyerezi Dar es Salaam. Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. 
Lengo kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi. 
Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa. Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
 Mhandisi wa Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita Yagela (Kulia) akiwaonesha michoro ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipotembelea eneo la ujenzi huo, Madimba, mkoani Mtwara. Wanaotazama ni wakaguzi hao, kutoka kushoto ni Prof. Longinus Rutasitara, Bibi Salome Kingdom, Bibi Florence Mwanri na Bw. Jordan Matonya.
 Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais ikijionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba, mkoani Mtwara.


  Vongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Prof. Longinus Rutasitara (Kushoto) na Bibi Florence Mwanri (Kulia) wakiangalia moja ya bomba la kusafirishia gesi. Bomba moja lina uzito wa tani tano na urefu wa mita 11. Mpaka sasa jumla ya kilomita 350 kati ya kilomita 492 zimeshatandazwa.
Mhandisi wa Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita Yagela (Kulia) akiwaonesha mabomba ya kusafirishia gesi Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipotembelea baadhi ya maeneo yanakopita mabomba hayo. Mpaka sasa jumla ya kilomita 350 kati ya kilomita 492 zimeshatandazwa.  
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa makazi ya wafanyakazi katika kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba, mkoani Mtwara. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Ni hatari mabomba yakiwa juu hivyo. Matatizo haya ndio yapo pia Nigeria. Naamini, wakandarasi wanalifahamu fika hili, ila nashangaa kwa nini wanafanya hivi.

    ReplyDelete
  2. Hata mie nashangaa maana wahujumu uchumi itakuwa rahisi kuchimbua na kutoboa matundu na kusababisha uharibifu wa mazingira, moto wa maangamizi kulipuka na hasara ya miundo mbinu ya usambazaji gesi. maana moto utafuata gesi mpaka Ubungo, DSM.

    ReplyDelete
  3. Anony March 27, 2014,
    Ondoa shaka Mdau. Bomba hazitokuwa juu, zitafukiwa.
    Angalia picha ya nne toka juu uone huo mfereji zitakapolazwa. Kimo cha shimo ni takribani futi sita kwenda chini.

    Mkabakuli

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...