Diwani wa Kata ya Endiamtu, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Zacharia akiwahamasisha wakazi wa kitongoji cha Kilimahewa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) baada ya diwani huyo kuwachangia sh 500,000 za kaya 50 za kata hiyo.

Ili kuwahamasisha wananchi wajiunge na mfuko wa afya ya jamii (CHF) Diwani wa Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Zacharia amelipia sh500,000 za gharama za matibabu, kwa kaya 50 za watu 300 wa kata hiyo.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa kitongoji cha Kilimahewa kilichopo katika kata hiyo, Zacharia alisema wananchi wengi wakijiunga na CHF, dawa na vifaa tiba vitapatikana kwa wingi kwenye kituo cha afya Mirerani.

Alisema kaya moja yenye baba, mama na watoto wanne wakichangia sh10,000 wanatibiwa kwa mwaka mmoja katika zahanati, kituo cha afya na hospitali kwenye wilaya husika hivyo jamii inatakiwa ichangamkie fursa hiyo.

“Ndugu zangu, maendeleo yetu Endiamtu kwa pamoja tunaweza, hivyo tujiunge kwa wingi kwenye mfuko huu ambapo watu wengi tukijiunga Serikali inatuunga mkono nusu kwa nusu na kuboresha kituo chetu cha afya,” alisema Zacharia.

Alisema endapo wananchi wakiweza kuchangia sh5 milioni kwenye mfuko huo, Serikali nayo inachangia sh5 milioni na wakichangia sh10 milioni, Serikali pia itachangia kiasi kama hicho hivyo mpango huo unamanufaa makubwa.

Hata hivyo, ili kumuunga mkono Diwani huyo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilimahewa, Joseph Masasi naye alijitolea sh100,000 kwa kaya 10 zenye baba, mama na watoto wanne wa kitongoji hicho, watakaotibiwa na mfuko wa CHF.

“Tunashukuru sana na tunampongeza diwani wetu Zacharia, ambaye ni mtu watu kwani kwa roho moja amejitolea sh500,000 kwa ajili ya kuwalipia watu wasio na uwezo wakiwemo wajane na yatima,” alisema Masasi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...