Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Vedastina Justinian akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Mradi wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts) unaolenga kurahisisha taratibu za forodha, uhamiaji, usimamizi wa ubora wa bidhaa, ulinzi na usalama. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Miundombinu ya Kiuchumi Mhandisi Abdillah Mataka na kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Frank Mvungi.

Mradi wa Vituo Vya Utoaji Huduma Kwa Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts – OSBP) unalenga kurahisisha taratibu za forodha, uhamiaji, usimamizi wa ubora wa bidhaa na huduma, usalama na ulinzi kwa kutoa huduma hizi upande mmoja wa mpaka kwa pamoja. Mradi umekamilika kwa baadhi ya Mipaka kama Holili, Mutukula na Sirari. Ujenzi wa Vituo vya Namanga, Horohoro na Rusumo uko katika hatua za mwisho.




Utekelezaji wa OSBPs pamoja na kuandoa utaratibu wa sasa ambapo aina zote za udhibiti zinazofanyika mpakani hufanyika mara mbili, shughuli zote za udhibiti zitaendelea kufanyika kwa ukamilifu  katika upande mmoja badala ya kulazimika kurudiwa katika upande wa pili wa mpaka kama ilivyo zoeleka.

Mradi huu unatekelezwa kwanza kwa kutunga Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuanzisha Vituo Vya Utoaji Huduma Kwa Pamoja Mipakani (OSBPs)  katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tayari Bunge la Afrika Mashariki lilipitisha Sheria hiyo mwezi Mei, 2013 na sasa iko katika hatua za kuidhinishwa na Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hatua ya pili ni ujenzi wa OSBPs hizo katika mipaka mbalimbali ambayo iko katika hatua  zifuatazo:

Holili/Taveta mpaka unaozitenganisha Tanzania na Kenya kwa upande wa Holili OSBP imekamilika na imekabidhiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ambao ndio waendeshaji wa OSBP zote nchini na upande wa Kenya mpaka wa  Taveta mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2014.

Katika Mipaka ya Sirari/Isebania unaozitenganisha Tanzania na Kenya kwa upande wa Mkoa wa Mara na Mpaka wa  Mutukula/Mutukula unaozitenganisha Tanzania na Uganda kwa upande wa Tanzania Vituo vimekamilika. Aidha, Ujenzi wa Kituo cha Namanga  ulioanza mwezi Desemba, 2011 kama sehemu ya Mradi wa barabara ya Arusha – Namanga – Athi River unaendelea.

Kituo cha Kabanga/Kobero kilichopo katika mpaka wa Tanzania na Burundi muda wa Mradi ni miezi 15 na ulianza mwezi Mei, 2013 na unatarajiwa kukamilika Juni, 2014, hatua ya ujenzi wake imefikia  20% hadi kufikia Februari, 2014.

Mradi wa ujenzi wa OSBP ya Rusumo mpaka uliopo kati ya Tanzania na Rwanda umefikia asilimia 69.5% upande wa Tanzania hadi kufikia mwezi Februari, 2014 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba, 2014.

Mradi huu pia unatekelezwa katika mpaka wa Horohoro/Lungalunga mpakani mwa Tanzania na Kenya kwa upande wa Mkoa wa Tanga, ambapo hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2013 ujenzi wa kituo hiki ulikuwa umekamilika 90% na ilitarajiwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, 2014 Mradi kuwa umekamilika.

Kwa upande wa Tunduma OSBP – kituo kinafadhiliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Trade Mark East Africa (TMEA) chini ya usimamizi wa TBA. Ujenzi bado haujaanza; TMEA wako katika mchakato wa kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la OSBP.

Rasimu ya Mkataba wa Ubia (Bilaterall Agreement) ya uendeshaji wa OSBPs kati ya Tanzania na Kenya imekamilika. Taratibu za kusaini Mkataba huu zinakamilishwa ili usainiwe hivi karibuni na kuwezesha Kituo kuanza kufanya kazi.
Ujenzi wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani utasaidia usafiri na usafirishaji wa haraka kwa kuondoa urasimu mipakani na hivyo kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji kwa Wanaafrika Mashariki.



Mkurugenzi Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi. Tumaini Mtitu akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam mikakati ya kudhibiti ubora wa bidhaa za ndani na zinazotoka nje ili kuepuka madhara kwa watumiaji  wa bidhaa hizo. Kushoto ni Afisa Uhusiano wa shirika hilo Bi Roida Andusamile.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...