Mawasiliano ya barabara kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo yamejifunga kutokana na barabara hiyo kubomolewa na maji katika Daraja la Mpiji mpakani mwa mikoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alifanikiwa kufika katika eneo hilo mara tu baada ya kupokea taarifa za kukatika kwa barabara hiyo. Akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Alhaj Mussa Iyombe pamoja na watendaji wengine kutoka TANROADS, Waziri Magufuli amewaagiza watendaji hao kuhakikisha kuwa wanafanyakazi mchana na usiku ili barabara hiyo muhimu na yeye kupitisha magari mengi ifunguliwe mapema iwezekanavyo.

Zaidi ya maelekezo hayo, Mhe. Magufuli pia ameagiza kuahirishwa hadi itakapopangwa baadaye kwa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika kuanzia siku ya Jumanne ya tarehe 15 Aprili 2014 huko mkoani Tanga. Hatua hiyo imechukuliwa ili watendaji hao wabaki katika vituo vyao vya kazi hadi hali ya mvua zinazoendelea kutulia na taarifa nyingine kutolewa.

Akizungumzia hali katika eneo hilo la Mpiji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Alhaj Mussa Iyombe kwa upande mwingine alibainisha kuwa kilichozolewa na maji ni sehemu ya barabara na siyo daraja lenyewe la Mpiji.

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali hapa nchini zimesababisha madhara kadhaa kwa upande wa miundombinu ya barabara. Waziri Magufuli ameendelea kutahadharisha kuhusu shughuli za uchimbaji wa mchanga zinazofanywa karibu au chini ya madaraja, kwamba kwa maeneo mengi ndicho chanzo cha mito kuhama kutoka katika njia yake ya asili na kubomoa barabara. “Kama manavyoona daraja lenyewe ni zima na linauwezo mkubwa wa kupitisha maji lakini mto umehama kutokana na uharibifu wa mazingira” alisistiza Mhe. Magufuli.

Daraja la Mpiji lilifunguliwa rasmi mwezi Julai 2005 na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati huo akiwa ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

TANROADS kwa kushirikiana na kampuni za ujenzi za SKOL na Estim Construction Company Limited zote za Dar es Salaam tayari wameanza kazi za kurekebisha sehemu hiyo.
Sehemu ya barabara iliyoomole katika Daraja la Mpiji kwenye barabara ya Dar es Salaam Bagamoyo.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akipokea maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wiara ya Ujenzi Alhaj Mussa Iyombe (aliyenyoosha mkono). Kulia ni Mbunge Mteule wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mbele wa kwanza kulia) akiongozana na Viongozi wengine wakati walipotembelea kukagua sehemu ya barabara iliyobomoka katika barabara ya Dar – Bagamoyo. Wengine kutoka kushoto ni; (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam) Suleiman Kova, (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam) Mhe. Said Mick saddik na (Mbunge Mteule wa Chalinze) Mhe. Ridhiwan Kikwete.
Sehemu ya barabara na daraja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. waswahili hapa huwa tunakosea,mtu akichaguliwa kwa kura sio mteule,ni mchaguliwa.mara tu baada ya uchaguzi utasikia rais mteule,mbunge au mwakilishi mteule.hao si wateule.mawaziri,wakurugenzi,wakuu wa vyombo vya usalama na ulinzi ndio wateule,hawapigiwi kura.Ridhwan mbunge aliechaguliwa,hakuteuliwa,si mbunge mteule.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...