Na Sultani Kipingo
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya inayowakabili watu wanne watano wakiwemo maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ya matumizi mabaya ya madaraka na kuingiza nchini vipimo feki vya kupimia virusi vya ukimwi na kuisababishia serikali hasara ya Sh.bilioni 3, umeomba mahakama kuhamia nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza Sylvester Matandiko kwa ajili ya kumsomea mashtaka yake.
Maombi hayo yaliwasilishwa jana na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa.
Swai alidai kuwa washtakiwa wengine wameshasomewa mashitaka bila Matandiko kuwepo mahakamani kwa madai kuwa ni mgonjwa kutokana na sababu hiyo, upande wa Jamhuri unaomba Mahakama kuhamia nyumbani kwa mshtakiwa huyo.
"Mheshimiwa hakimu, niliongea na mke wa mshtakiwa kwa njia ya simu na akanijibu kwamba hali yake siyo mbaya sana na kwamba tatizo kubwa hana uwezo wa kutembea umbali mrefu... ni rai yetu Jamhuri kuhamishia mahakama nyumbani kwa mshtakiwa ili aweze kusomewa mashitaka yanayomkabili" alidai Swai.
Hata hivyo, upande wa utetezi uliomba mahakama kama ikiamua kufanya hivyo iwe kwa tahadhali kutokana na hali ya mshitakiwa kuwa bado kuimarika kwa sababu anasumbuliwa na maradhi ya kiharusi.
Hakimu Riwa alisema kesi hiyo itatajwa tena Mei 30, mwaka huu.
Mbali na Matandiko ambaye ni Mkurugenzi wa Oparesheni Kanda ya Kaskazini wa MSD, wengine ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa MSD, ambaye pia ni Meneja wa Viwango, Sadiki Materu, Wasajili kutoka Bodi ya Maabara za Afya ni Zainabu Mfaume na Joseph Nchimbi.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja, wanakabiliwa na mashtaka saba, ya kutumia madaraka vibaya, na hivyo kuisababishia hasara Serikali ya dola za Marekani 2,093,500, kwa kuruhusu uingizaji wa vitendanishi feki vya HIV nchini, na kuingizwa Bohari Kuu ya Dawa.
Swai alidai kuwa katika shitaka la kwanza, washtakiwa wote, kati ya Januari 20 na Julai 20, 2012, walikula njama ya kutenda kosa la kutumia madaraka yao vibaya kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Alidai katika shitaka la pili dhidi ya Matandiko ambaye hakuwepo mahakamani hapo, kwamba Februari 3, 2012, katika ofisi za MSD iliyopo wilayani Temeke, Dar es Salaam, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuruhusu Bodi ya Maabara za Afya kupitia barua yenye kumb. MSD/003/2011/2012/390 ya Februari 3, 2012 kutoa kibali kwa Kampuni ya SD Africa, kuingiza vitendanishi vya HIV SD Bioline ½ 3.0 feki vilivyotengenezwa na Standrd Diagnostics ya Korea vilivyozuiliwa na Serikali kuingizwa nchini.
Aidha, ilidaiwa kwamba kwa kufanya hivyo, Kampuni ya SD Africa ilipata faida ya dola za Marekani 2,093,500, sawa na zaidi ya Sh.bilioni 3.
Swai alidai katika shitaka la tatu kwamba mshtakiwa Zaynabu na Sadiki, Januari 17, mwaka 2012, katika ofisi za Bohari Kuu ya Dawa, walitumia madaraka yao vibaya kwa kumshauri Naibu Mkurugenzi wa itifaki, kukubali Kampuni ya SD Africa kuingiza vipimo hivyo feki na kujipatia kiasi hicho cha fedha na kuvisambaza MSD.
Shitaka la nne linamhusu mshtakiwa Sadiki, ambaye anadaiwa kwamba Februari 29, mwaka 2012, katika ofisi za Bohari Kuu ya Dawa, aliidhinisha ubora wa vipimo hivyo vilivyozuiwa na Serikali kuingia nchini, na hivyo kusababisha Kampuni ya SD Africa kujipatia fedha hizo.
Shtaka la tano linamkabili Nchimbi, anayedaiwa kwamba Februari 7, mwaka 2012, akiwa Bodi ya Maabara za Afya, alitumia madaraka vibaya kwa kupitisha hati ya malipo namba SD111225-20 ya Desemba 25, mwaka 2012 na SD120109-3 ya Januari 9, mwaka 2012 kwa ajili ya kuingiza vipimo hivyo feki.
Katika shitaka la sita ilidaiwa kuwa Zaynabu kupitia cheo chake alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa cheti cha kuingiza na kusafirisha bidhaa mbalimbali za afya za maabara namba 00010131, cha Februari 7, mwaka 2012, ili kuingiza vipimo hivyo feki.
Swai aliendelea kudai kuwa shitaka la saba linawakabili washtakiwa wote, katika vipindi hivyo, waliisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 3 kwa kuingiza vipimo hivyo feki vilivyozuiliwa na Serikali ya Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...