Wakati Serikali ikiwa katika jitihada za kuhakikisha kuwa inajiongezea mapato ili kuweza kuwahudumia vyema wananchi wake, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) utasaidia kuongeza takribani Sh. trilioni 3.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Ukusanyaji Fedha kutoka Ofisi ya Rais-Usimamizi wa Utekelezaji wa Miradi (PDB), Lawrence Mafuru alipohojiwa katika kipindi cha Makutano Show kinachorushwa na Radio Magic FM.
PDB ni kitengo kipya kilichoanzishwa chini ya Rais kusimamia Mpango wa BRN ili kuchagiza ufanisi wa kasi na viwanbgo katika sekta sita zilizochaguliwa na elimu, maji, kilimo, Nishati, usafirishaji na ukusanyaji wa fedha.
"Katika eneo la ukusanyaji wa fedha, BRN, imekuja na mtazamo mpya na mikakati mipya. Tunaamini kuwa zipo njia mpya za kikodi na zisizo za kikodi ambazo zinaweza kuliongezea Taifa mapato na tumejiwekea lengo hilo la trilioni 3," Bw. Mafuru alisema.
Aliongeza kuwa ili kuongezeka kwa mapato ya Serikali Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itafanyakazi kwa karibu na PDB kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa.
Aliutaja mkakati mwingine wa kufikia hilo ni kuhakikisha makampuni ya umma ambayo yanazalisha faida yanalipa gawio kwa Serikali na pia kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi.
Naye Bw. Mugisha Kamugisha kutoka PDB, alisisitiza kuwa BRN imejiwekea malengo Makubwa ili kila mhusika atimize wajibu wake.
"Ukiyaangalia malengo na miradi mikubwa iliyopangwa kusimamiwa chini ya BRN, utaona kuwa baadhi ni magumu kufikiwa. Lakini sisi tunaamini kuwa huwezi kuona umuhimu wa kujituma mpaka pale kujituma kunapobaki ni jambo pekee unalopaswa kulifanya," alisema Bw. Kamugisha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...