Mshauri wa Masuala ya Maendeleo ya Jamii na Mahusiano; wa Kampuni ya BG Tanzania, Emil Karuranga (wa pili kushoto) na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Africare, Alfred Kalaghe (wa pili kulia) wakisaini mkataba wa makubaliano wakati wa uzinduzi wa Mradi wa mafunzo kuwawezesha vijana kiuchumi mkoani Mtwara juzi. Wanaoshuhudia (kulia) ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Johansen Bukwali na Meneja Mradi wa vijana, Dickson Mbita.
Kampuni ya BG kwa kushirikiana na Kampuni ya Africare Tanzania wamezindua Rasmi mradi wao wa kuwawezesha vijana unaoitwa "Kijana Jikwamue"Mkoani Mtwara. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia ndiye mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi huo.
Mradi huo una lengo la kuboresha maisha ya vijana katika Wilaya ya Mtwara kupitia mafunzo ya ujasiriamali, ushauri na stadi za maisha.
Kampuni ya BG imedhamiria kutumia dola za Kimarekani 765,000 takribani shilingi za Tanzania, Bilioni 1.23 zitakazowekezwa kwa kipindi cha miaka mitatu, ikiendelea kujitoa kwa kujenga na kutoa fursa zitakazo wasaidia watu kuwa na uwezo kuboresha maisha yao katika ngazi ya chini mpaka ngazi ya Kitaifa.
Akizungumza katika tukio hilo, Kanali Simbakalia alisema"Vijana ni uti wa mgongo wa Taifa na tunawashukuru Kampuni ya BG Tanzania kwa kudhamini mradi huu, Sisi kama serikali tunawahakikishia kwamba mradi huu utakuwa endelevu na utainufaisha jamii. Tunatoa wito kwa makampuni mengine ya gesi na mafuta kuwekeza zaidi kwenye programu za vijana hasa kwenye eneo la ujasiriamali na kuwajengea uwezo."
Lengo la mradi huo ni kuwasaidia vijana kuwaelimisha kuhusu dhana ya ubunifu ya ujasiriamali na mipango ya kuwawezesha kuanza au kupanua biashara zao, na kujenga fursa za ajira kwa jamii zao. BG na Africare wameshabainisha vikundi vya ujasiriamali, mahali walipo na aina ya shughuli za kiuchumi wanazofanya katika mkoa wa huo.
Mshauri wa Masuala ya Maendeleo ya Jamii na mahuisiano; Kampuni ya BG Tanzania, Bwana Emil Karuranga, amesema, " BG Tanzania inaamini kwamba ufunguo muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ipo katika kujengea uwezo wadau kwenye maeneo mbalimbali. Kuwekeza katika mtaji wa rasilimali watu ni njia bora ya kukuza uchumi na maendeleo ya watu kwa ujumla. Uwezeshaji wa vijana ni kipaumbele chetu kwa sababu wao ni tegemeo la siku za baadaye kwa nchi ya Tanzania ".
Akizungumza kwa niaba ya Africare Tanzania, Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo, Bwana Alfred Kalaghe alisema , " Africare imefurahishwa kuona BG Tanzania wametenga fedha kusaidia mradi wa vijana. Mradi huu utasaidia kuongeza kipato kupitia kuongezeka kwa ajira, Africare inaamini kwamba kama vijana watahimizwa kushiriki katika shughuli zitakazo boresha hali za maisha yao, basi watakuwa na uwezo wa kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wake "
Mradi huu ni moja kati ya jitihada za BG Tanzania katika kujenga uwezo, kama vile, ufadhiri wa mafunzo stadi wa chuo cha ufundi cha VETA katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...