Na Mahmoud Zubeiry
KAMA ilivyotarajiwa, Michael Richard Wambura (pichani) ameenguliwa katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi mkuu wa Simba SC unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, kwa sababu kubwa mbili.
Akizungumza katika Mkutano maalum na Waandishi wa Habari mchana huu makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), makutano ya mitaa ya Ohio na Libya, Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, Wakili Dk Damas Daniel Ndumbaro amesema Wambura ameondolewa kwa sababu kwa sasa si mwanachama halali wa klabu hiyo.
Wambura alisimamishwa uanachama wa Klabu ya Simba tangu Mei 5 mwaka 2010 kutokana na kosa la kuipeleka klabu hiyo mahakamani akifungua kesi namba 100 ya mwaka 2010 katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, Dk Damas Ndumbaro kulia akifafanua jambo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo. Kushoto ni Katibu wa Kamati, Issa Batenga


Ndumbaro amesema kuwa Wambura aliwasilisha barua pia katika Kamati ya Uchaguzi akikiri kuipeleka Simba mahakamani na kuiomba Kamati hiyo kumaliza suala lake na kuahidi hatarudia tena kufanya kosa kama hilo, amepingana na Katiba ya klabu, TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Mwenyekiti huyo wa Kamati amesema kwamba pia walipokea barua mbili tofauti kutoka kwa Wambura ya kwanza ikiwa ya Novemba 6 mwaka 2012 mgombea huyo akitaka kujua uhalali wa uanachama wake na nyingine ya Septemba 15 ikijibu kuwa Simba haina tatizo lolote na yeye.
“Kuna utata katika barua zake na pia kuna barua ya tatu ya Septemba 25 mwaka 2012 ikieleza pia  Simba hawana tatizo na Wambura,” amesema Ndumbaro.
Aliongeza kuwa kutokana na Kamati yake kujiridhisha na maelezo hayo, imeamua kumuondoa Wambura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Ndumbaro ameeleza zaidi kuwa kutokana na maamuzi ya kusimamishwa huko, Wambura hapaswi kushiriki katika shughuli za Simba kwa mujibu wa Ibara ya 12(3) ya katiba ya klabu hiyo ya mwaka 2010 na ibara ya 12(3) ya 2014.
Alieleza kuwa endapoa Wambura hataridhika na maamuzi hayo anaruhusiwa kukata rufaa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF.
Ndumbaro amesema pia wagombea wengine wote walioekewa pingamizi wamepitishwa na wataendelea na mchakato wa uchaguzi huo utakaofanyika Juni 29 mwaka huu.
Kwa kuondolewa Wambura, nafasi ya wagombea Urais inabaki na watu wawili, ambao ni Evans Elieza Aveva na Andrew Peter Tupa, wakati wanaowania Umakamu wa Rais ni Jamhuri Kihwelo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na Swedi Nkwabi.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Wambura amesema kwamba atazungumza kesho katika Mkutano na Waandishi wa Habari, kwa leo hakuwa tayari kuzungumza na mtu mmoja mmoja. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. wamemuonea, utafiki kauwa mtu.pe

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 28, 2014

    Katika picha mjumbe huyo si ni mwanachama wa Bwawa la Maini a.k.a Liverpool sasa watasemaje kuwa huyu mgombea mtarajiwa siyo mwanachama halali wa Simba Sc.

    Mdau
    Mtani Jangwani.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 28, 2014

    Tena..? Huyu jamaa basi tishio namshauri ajaribu shughuli nyingine maana pengine milango inaweza kufunguka lakini huko!

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 28, 2014

    Nampongeza M/Kiti wa kamati ya hii ya uchaguzi na pia nawapongeza sana sana, wanachama na wapenzi waliomwekea pingamizi Wambura kwa kuonyesha kwa vitendo machungu yao, kwamba wameona mbali katika maendeleo ya soka la nchi hii. Wambura, sio tu HAFAI kuongoza Simba, bali ofisi na taasisi yoyote ya soka au michezo kwa ujumla hapa nchini. Ni funzo kwake kwamba watu hatujasahau alivyotupa mateso alipokuwa TFF au FAT wakati huo. Wambura ni mtu wa migogoro, kwa mliosahau, kumbukeni jinsi tasnia ya soka ilivyojaa migogoro wakati wa enzi zake, labda yeye kasahau lakini sisi bado tunakumbuka sana, tena kwa machungu. Huyu ni mtu wa kuogopwa sana katika soka.

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 28, 2014

    Alikwenda mahakamani wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za soka na adhabu yake inajulikana kwa hiyo anatakiwa akubali matokeo yake. Aliamua mwenyewe kujiondoa ktk familia ya soka!!

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 28, 2014

    Natamani ningekuwa na uwezo nimwaajiri huyu jamaa, lazima awe potential sana huyu. Jamani kichwa hicho kifanyieni kazi badala ya kukipiga danadana.

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 29, 2014

    maneno maneno tu... mbona wengine mpaka jela wakaenda na bado mkawachagua. acheni chuki binafsi mpeni nafasi wambura angalau aenguliwe kwenye kura na si vinginevyo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...