Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kushirikiana na Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) kitafanya Mkutano wake Mkuu wa 12 utakaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC), Arusha, Tanzania.
Mkutano huo wa Kimataifa ambao utashirikisha jumla ya Majaji Wanawake takribani 600 kutoka nchi mbalimbali duniani wakiongozwa na Rais wao ambaye ni Mtanzania, Mhe. Eusebia Munuo, Jaji wa Rufaa (Mstaafu), utaanza rasmi mnamo tarehe 05 Mei, 2014 na utafunguliwa na Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maudhui ya Mkutano huo muhimu ni: ‘Justice for All’ ikiwa na maana ya‘Haki kwa wote’
Aidha; Mkutano huo utatoa fursa ya kupanua wigo wa mawasiliano kati ya Majaji Wanawake duniani ili kujenga mazingira mazuri ya utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kujenga ubora na uadilifu katika utoaji haki na ukuzaji (promotion) wa Haki za Binadamu.
Mkutano huo ambao utadumu kwa muda wa wiki moja utafungwa rasmi na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe Balozi Seif Alli Iddi.
Wakiwa hapa nchini wajumbe wa Mkutano huo watapata fursa pia ya kufanya utalii kwa kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo Mkoani Arusha.
Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) kiliundwa rasmi mwaka 1991.
Chama hiki kina Makao Makuu yake huko Washington DC nchini Marekani. Chama hiki kina jumla ya wanachama takribani 4,000 kutoka katika nchi zisizopungua 100 ambapo wanachama wake wanatoka katika kila ngazi ya Mahakama duniani.
Chama kinafanya kazi kwa karibu na Wanachama wake kuhakikisha kuwa:-
• Wanashirikiana na Taasisi na vyama vingine katika masuala ya upatikanaji wa haki sawa.
• Kutoa elimu kuhusiana na masuala ya haki za binadamu na jinsi wanawake wanavyoweza kupata huduma za Mahakama n.k.
• Kuendeleza mtandao wa Kimataifa wa Majaji Wanawake na kutengeneza fursa za kubadilishana uzoefu kuhusu utawala wa sheria kupitia mikutano ya Kimataifa, Mafunzo, vijarida n.k.
Imetolewa na : CHAMA CHA MAJAJI WANAWAKE TANZANIA (TAWJA).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...