Marehemu Maximilian John Ngube enzi za uhai wake
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari Mheshimiwa
Dkt.Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mpiga picha wa kituo cha television cha
Mlimani, Ndugu Maximilian John kilichotokea alfajiri ya kuamkia leo tarehe 24
Mei,2014.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Bwana Maximilian
kilichotokana na maradhi ya Moyo, Sukari na Shinikizo la damu. Kifo hicho ni pigo
na pengo kubwa kwa tasnia ya habari hapa nchini,”Amesema Rais Kikwete katika
salamu hizo.
“Bw. Maximilian atakumbukwa kwa uchapakazi wake na uhodori katika kazi zake
siku zote. Kifo ni maandiko ya Mwenyezi Mungu hivyo hatuna budi kumshukuru kwa
yote.
“Nakutumia salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako,
naitumia familia ya Ndugu Maximilian, pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa
na mzazi na mhimili wa familia. Aidha, salamu hizi ziwafikie pia wanahabari wote,
wafanyakazi wenzake, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu. Nakuomba uwajulishe
kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu.
Ninaungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi
roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo.
Ndugu Maximilian John ameacha mke na watoto wanne.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
24 Mei,2014
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...