Na Mwandishi Maalum 
 Tanzania inaweza kuongeza zaidi kasi yake ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake, kwa kujifunza uzoefu wa nchi nyingine marafiki kama vile Uhispania. Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, ameyasema hayo siku ya jumanne, wakati alipokuwa akichangia majadiliano ya mada kuhusu “Kuendelea kwa Pamoja: misaada ya maendeleo ( ODA), biashara na uwekezaji”. 
Muwasilishaji wa mada hiyo alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Uhispania, Bw. Jose Manuel Garcia- Margallo Y Marfil, alipokutana na kubadilishana mawazo na Balozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa. 
Balozi Manongi amesema katika majadiliano hayo, kwamba Tanzania kama nchi inaaamini kuna maeneo ambayo inaweza kujifunza zaidi na kutumia uzoefu wa Hispania katika kusukuma mbele kasi ya ukuaji wa uchumi wake na maendeleo. 
 Akabainisha kuwa maeneo ambayo Tanzania kwa kushirikiana na Uhispania inaweza kujifunza na kubadilishana uzoefu ni uwekezaji, biashara na uvutiaji wa misaada ya maendeleo. 
“Tanzania inapenda kukushukuru kwa kuadaa mkutano huu na fursa hii ya kubadilisha mawazo kuhusu dhana nzima ya maendeleo ya pamoja, misaada ya maendeleo, biashara na uwekezaji
“Maeneo haya ni muhimu sana kwetu na nina amini tunaweza kubadilisha uzoefu na kujifunza namna ambavyo nyinyi mumefanikiwa” akasema Balozi.
Aliongeza kwamba hata katika majadiliano yanayoendelea hivi sasa kuhusu ajenda mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015, maeneo yanayotiliwa mkazo mkubwa pamoja na mambo mengine , ni hayo ya uwekezaji, biashara na misaada ya maendeleo. 
“ Ni kwa kutumia fursa zilizopo za uhusiano baina ya nchi na nchi na ushirikiano katika ngani ya kimataifa, tunaweza kuendelea kwa pamoja”, akaongeza Balozi Manongi 
Aidha Mwakilishi huyo wa Tanzania kama ilivyokuwa kwa wawakilishi wengine waliochangia majadiliano yao, akatumia fursa hiyo kuishukuru Uhispania, kwa uamuzi wake wa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo Endelevu kwa ubia na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa ( UNDP). 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Uhispania, pamoja na mambo mengine, aliwaeleza mabalozi kwamba, nchi yake ambayo ilikumbwa na mtikisiko mkubwa wa kuyumba kwa uchumi angalau imeanza kutengemaa kwa kuchukua hatua kadhaa wa kadhaa, ingawa amekiri kwamba safari bado ni ndefu. 
Baadhi ya mambo ambayo anasema serikali yake iliamua kuyafanyia kazi kwa kuyapa umuhimu ni pamoja na, kufungua milango ya uwekezaji ndani na nje ya nchi yake, kukuza na kupanua biashara na upatikanaji wa ajira kwa vijana wao. 
Akabainisha kwamba kama si kupanua wigo wa biashara, kuongeza kasi ya uwekezaji ndani na nje, Uhispania isingeweza kujifunia mafanikio iliyonayo hivi sasa ikiwa ni pamoja na kuyatafsri mafanikio hayo katika ushirikiano wa kimaendeleo. 
 Na kwa sababu hiyo akasema nchi yake imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa misaada ya maendeleo kwa nchi mbalimbali yenye uhusiano nao ikiwa ni pamoja Umoja wa Mataifa. Akatoa mfano kwa kusema kati ya 2007 na 2012 nchi yake imechangia zaidi ya dola za kimarekani 30 billion kwenye eneo la maendeleo, misaada ambayo ilitolewa kupitia uhusiano baina yake na nchi nyingine na katika ngazi ya kimataifa. 
Ambapo Afrika Kusingi mwa Jangwa la Sahara ilipata jumla ya dola 4 billioni kama msaada wa maendeleo. Kuhusu uwekezaji akasema nchi yake inamtaji wa dola bilioni 640. Vile vile Uhispania ni nchi ya saba kama msafirishaji wa huduma katika nchi mbalimbali na ni ya 17 kama msafirishaji mkubwa bidhaa. 
 Akasema ni katika kuamini kwake katika dhana nzima ya ushirikiano wa kimaendeleo ndio maana nchi yake licha ya kutoa misaada kwa nchi moja moja na katika ngazi ya Umoja wa Mataifa, ndiyo maana imeamua kwa kushirikiana na UNDP kuunda mfuko wa maendeleo endelevu kama ilivyofanya kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Millenia ( MDGs). 
Akasisitiza kwamba nchi yake imeamua kuunda mfuko huo kwa kile inachoamini kwamba utakuwa daraja au kiungo kati ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia ambayo yanaishia ukiongoni, na malengo mapya ya maendeleo endelevu.
Sehemu ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa, wakati wa majadiliano  kuhusu dhana ya  maendeleo ya pamoja,  uwekezaji, biashara na misaada ya maendeleo,  majadiliano hayo yaliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Uhispania, Bw.Jose Manuel Garcia- Margallo Y Marfil ambapo pia alielezea nafasi ya nchi yake katika  kukuza  ushirikiano na  misaada  ya kimaendeleo  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...