Na Waandishi Wetu, Arusha
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuyapa uzito matukio yanayowatokea waandishi wa habari na kuyapigia kelele kwa nguvu zote ili kuyakomesha.
Kibanda aliyasema hayo jana mjini Arusha katika kongamano lililoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani na kuongeza kwamba wakati umefika kwa waandishi wa habari kuondoa tofauti zao na kuungana pamoja kuongeza nguvu waliyonayo kukabiliana na ukatili unaoendelea dhidi ya waandishi wa habari katika miaka ya hivi karibuni.
“Baadhi ya wahariri huwa hawayaandiki madhila yanayowasibu waandishi wa habari na kuyapa uzito unaostahili aidha kwa huyapuuzia au kudharau kwa kuwa hayawahusu moja kwa moja,” alisema Kibanda.
Aliongeza kwa kusema kuwa vyombo vya habari mara nyingi vimekuwa vikinyooshewa vidole na kulaumiwa kwa kutokufanya kazi kwa uadilifu jambo ambalo linatafsiriwa kuwa ni la uonevu, vinatumiwa vibaya na hakuna anayesimama kuvitetea kutokana na mchango wake mkubwa katika jamii.
Afisa Mipango Kitengo cha Mawasiliano, Habari na Tehama UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph, akiwasilisha mada kuhusu mchango wa uhuru wa vyombo vya habari katika utawala bora, kukuza uwezo na kupunguza umaskini kongamano la waandishi wa habari lilioandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayofanyika jijini Arusha.
“Kwa sasa tasnia hii iko kwenye wakati mgumu sana kwani hata marais wa nchi mbalimbali mfano Uganda, Kenya hata Marekani wanakinzana na vyombo vya habari kwa madai kuwa kauli zao zinapotoshwa, laikini ukweli ni kwamba ni vyema kauli hizo za viongozi zikachunguzwa kwa undani zaidi ili kuelewa iwapo zina uwajibikaji ndani yake,” alisema Kibanda.
Kibanda aliongeza kuwa wakati umefika sasa kwa waandishi kutambua kuwa kuna ajenda za siri zilizojificha dhidi ya uteswaji wa waandhishi wa habari hivyo yasidharauliwe, yafanyiwe kazi kwa kina ili kuelewa kiini cha tatizo kwa kupata ufumbuzi.
Kwa upande wake mwandishi mkongwe na aliyetunukiwa tuzo ya maisha mwaka 2012 na Baraza la Habari Hamza Kasongo alisema vyombo vya habari vina nguvu kubwa katika kushawishi hivyo vitumie nguvu hiyo kama muhimili wa nne wa nchi katika kuzikabili changamoto zilizopo.
“Kuwe na mtandao unaoeleweka wa mawasaliano kati ya waandishi wa habari nchini ili kuhakikisha kuwa matatizo yaliyopo yanatatuliwa bila woga na kwa ujasiri kwa lengo la kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” alisema Kasongo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria , Bw. James Jesse, akitoa mada kuhusu umuhimu wa sheria katika kulinda haki ya uhuru wa kujieleza kwa kila mtu wakati wa kongamano la waandishi wa habari lilioandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yanayofikia kilele leo jijini Arusha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...