Na Rocky Setembo – Afisa Habari, Tume ya Maadili ya Viongozi.

Viongozi wakuu kutoka Chuo cha Biashara ‘CBE’ wameaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kusimamia uadilifu wa Chuo hicho ili kuhakikisha Taifa linapata wasomi waliojengeka vyema kielimu na kimaadili.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Viongozi wa Umma, Ofisi ya Rais - Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Tixon Tuyangine Nzunda, wakati akitoa Mafunzo ya Maadili kwa Wakurugenzi Wakuu na Wakurugenzi Wasaidizi, kutoka Kanda zote, wakiongozwa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Emanuel Mjema, jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.

Alisema uadilifu na uwajibikaji katika Utumishi wa Umma, hususani katika eneo muhimu kama la Elimu, husababisha kuondoa au kupunguza migongano mibovu ya kimahusiano kazini, matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kuleta tija na kuongeza thamani ya Elimu ya juu nchini, hali ambayo itaongeza ufanisi na udhibiti wa mianya ya ukiukwaji wa maadili na rushwa nchini.

Aliongeza kuwa, uongozi ulioadilifu hujenga ujasiri wa kusimamia sheria, kanuni na utaratibu bila uoga wala upendeleo, hivyo, ili waongozwao waende katika mstari uliosawa, yawabidi Viongozi wawe mfano bora na kioo kwa jamii.

“Kiongozi muadilifu huwa ni mfano katika kuleta mabadiliko. Awali, Chuo hiki cha Biashara, ambacho ni moja kati ya vyuo vikongwe nchini, kilikuwa hakina sifa sana hususani kwa upande wa wanachuo kuwa huru kuvaa vyovyote vile watakavyo. Hivi sasa, chuo hiki kimekuwa mfano wa kuigwa, hii ni kutokana na kuwepo na Uongozi uliobora na adilifu ambao umethubutu na umeweza kwa asilimia kubwa kukiweka chuo hiki katika hali iliyobora, kiuadilifu na kitaaluma. Hii ni hatua nzuri sana, na ni mfano wa kuigwa kwa vyuo vingine nchini” Alisisitiza Bw. Nzunda.

Awali, akifungua mafunzo hayo ya siku mbili, Mkuu wa Chuo cha “CBE” Profesa Emanuel Mjema alisema, lengo la kuyapokea na kuratibu mafunzo hayo ni kwanza kupata uelewa kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na matakwa yake, pili kupata muongozo uliobora utakaosaidia kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Maadili ya Chuo hicho.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoratibiwa na Chuo hicho, yalihusisha Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kitengo cha Uratibu, Utawala Bora - Ikulu na Kitengo cha Sheria cha Chuo cha Biashara - CBE.
Mratibu Msaidizi kutoka Kitengo cha Uratibu,Utawala Bora, Ikulu, Bw. Emanuel Mwanga akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Chuo cha Biashara – CBE.
Katibu Viongozi wa Umma, kutoka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma,Bw. Tixon Nzunda, akiwasilisha mada kwa Viongozi wa Chuo cha Biashara – CBE.
Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE) Profesa Emanuel Mjema (mwenye suti nyeusi) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Chuo hicho na Wawezeshaji mara baada ya Mafunzo ya Maadili, yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Viongozi wa Umma, Bw. Tixon Nzunda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...