Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe leo mchana amekutana na Waziri Mwandamizi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ndani wa Singapore, Masagos Zulkifli kuzungumzia Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini ofisini kwake Ubungo Maji Dar es Salaam.
“Tunatekeleza miradi mikubwa mitatu Nchini, mmojawapo ni ujenzi wa Bwawa kubwa la Kidunda, mkoani Morogoro ambalo litasaidia kuongeza upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam kwa miaka 20 ijayo,” alisema Waziri Maghembe.
“Hivyo, tunahitaji Ushirikiano wa Taasisi za Kibinafsi na Kiserikali kwa Maendeleo ya Kiuchumi Nchini (PPP) katika kuhakikisha tunatekeleza miradi ya maji na kuinua sekta hii, maana kutegemea bajeti ya Serikali pekee haitoshelezi kufikia malengo makubwa tuliyojiwekea kama Wizara.” alisisitiza Prof. Maghembe.
Pia, Waziri Maghembe alizungumzia changamoto tatu kubwa zinazoikabili Wizara yake katika kuhakikisha maji yanafika katika kila nyumba kwa wakazi karibu milioni 3.3 wa Dar es Salaam, ujenzi wa miundombinu ya majitaka na upotevu wa maji na kusisitiza ni jambo la kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Maghembe alimuomba mgeni wake kuhakikisha nchi yake inawekeza katika Sekta ya Maji ambayo ni muhimu katika nchi hii, na ikizingatiwa eneo la Kusini mwa Tanzania linategemea kushamiri kwa viwanda na wingi wa watu baada ya kugundulika gesi na hivyo uhitaji wa maji utaongezeka kwa kasi.
Aidha, Waziri wa Singapore, Masagos Zulkifli alisema watahakikisha wanawekeza na kuleta maendeleo katika sekta ya maji na kutumia wataalamu na uzoefu walionao kutoka nchi yao. Huku akisisitiza kufanikisha zoezi la uunganishaji mabomba kwa kila nyumba, kujenga miundombinu ya majitaka nchi nzima na upotevu wa maji.
Waziri huyo wa Singapore aliambatana na ujumbe mkubwa uliojumuisha wataalamu mbalimbali wa sekta tofauti nchini humo, ambao wapo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tano.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe akiwa na mgeni wake, Waziri Mwandamizi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ndani wa Singapore, Masagos Zulkifli wakielekea kwenye chumba cha mkutano.
Baadhi ya wataalam waliombatana na ugeni kutoka Singapore uliomtembelea Prof. Maghembe.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akiwa na, Waziri Mwandamizi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ndani wa Singapore, Masagos Zulkifli (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Bashir Mrindoko (kulia).
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe na Waziri Mwandamizi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ndani wa Singapore, Masagos Zulkifli, wakibadilishana zawadi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...