Na Richard Bagolele-Chato.
Wafugaji wa Ngo’ombe Wilayani Chato mkoani Geita wameaswa kuachana na ufugaji wa mazoea na badala yake wafuge kisasa zaidi.
Wito huo umetolewa leo Wilayani hapa na Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Rodrick Mpogolo wakati akifungua kikao cha pamoja na wafugaji wa Ng’ombe na wataalam wa mifugo ambacho pia kilidhuriwa na mwekezaji wa kiwanda cha kusindika nyama kutoka jijini Mwanza cha Chobo Investiment.
Mkuu wa Wilaya ya Chato amesema wafugaji wengi nchini wamekuwa wakufuga Ng’ombe wengi pasipo kupata mafanikio yoyote maishani jambo ambalo amelikemea na kuwataka wafugaji kufuga mifugo kidogo kwa njia ya kisasa zaidi ambapo mafanikio yataonekana, “ tuwe na program za kumwendeleza mfugaji, mpango wa kufuga mifugo wachache wenye tija badala ya kuwa na kundi kubwa la Ng’ombe linaloongeza migogoro kila kukicha, tunataka mifugo iwasaidie wafugaji kujiongezea kipato, kusomesha watoto, kuwa na malazi mazuri na maisha bora kwa ujumla” alisistiza Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine mwakilishi wa kampuni ya uwekezaji ya Chobo Investiment kutoka Mwanza Bw. Denis Kisoka amewahakikishia wafugaji wilayani chato uwepo wa soko la uhakika wa Ng’ombe waliofugwa kisasa ambapo hadi sasa amesema nyama inayozalishwa nchini Tanzania bado haijakidhi vigezo kutokana na ufugaji wa mazoea na hivyo kufanya kampuni yake kushindwa kuzalisha nyama inayokidhi soko hasa kwa baadhi ya wawekezajia wa kigeni waliopo hapa nchini.
Amesema kampuni ya Chobo Investiment wako tayari kutoa elimu kwa vikundi vya wafugaji vilivyoko wilayani Chato ili waweze kuzalisha mifugo bora na kukidhi mahitaji ya soko la nyama ambapo kipato cha mfugaji pia kitaongezeka.
Nao baadhi ya Wafugaji waliochangia kwenye kikao hicho wameitaka serikali kuboresha miundombinu kwa wafugaji hasa upatikanaji wa majosho na elimu ya ufugaji wa kisasa. Wafugaji hao wamesema uwepo wa maduka mengi ya dawa za mifugo husababisha miundombinu inayojengwa na serikali kutokutumika kutokana na wataalamu wa mifugo kujihusisha na biashara hiyo.
Bw. Noel Shadrack mfugaji toka kijiji cha Buzirayombo amesema wafugaji wakiamua kufuga kisasa wanaweza kwani ameshuhudia kwenye baadhi ya minada ya Ngo’mbe hapa Wilayani Chato wakiuzwa kwa shilingi 1,000,000 hadi 1,500,000 tofauti na bei ndogo zilizozoeleka za shilingi 150,000 hadi 300,000.
Nao baadhi ya watalaamu wa mifugo wilayani Chato wamewalaumu baadhi ya wafugaji kwa kufuga kwa mazoea na kuongeza kuwa baadhi ya wafugaji hawako tayari kupokea ushauri wa wataalamu eti tu kwa sababu wataalamu hao hawafugi chochote.
Wamesema kutokana na wilaya kutokuwa na maeneo makubwa ya malisho ya wanyama ni vyema wafugaji hasa wa Ngo’ombe wakafuga kidogo ili kukabiliana na tatizo hilo.
Kikao hicho cha siku moja kilikuwa na lengo la kumtambulisha mwekezaji wa usindikaji wa nyama kutoka Mwanza Chobo Investiment kimemalizika na kutoka na maazimio ya kuunda vikundi vya wafugaji kutoka vijijini ili waweze kupata elimu ya ufugaji bora na wa kisasa.
Wilaya ya Chato inakadiriwa kuwa na Ng’ombe wa asili zaidi ya 115,000 ambapo ufugaji huria umekuwa ukitumika katika maeneo yote wilayani hapa.
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Rodrick Mpogolo akiongea na wafugaji na wataalamu wa mifugo kutoka Chato
wafugaji na wataalamu wa mifugo wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chato wakati akifungua kikao hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...