
Mimi sina mfanyakazi wa jina hilo la Mariamu. Wala sina
mfanyakazi mwenye umri wa miaka 16. Hatuna tatizo lolote la mfanyakazi
yeyote kupigwa, achilia mbali kuuawa. Lakini taarifa hizo ambazo ni za uongo mtupu zimewashtua
wengi kwa sababu zimejengwa katika misingi ya chuki za kidini. Mwandishi
alilenga kuifanya jamii iamini kwamba mke wangu ambaye ni Mkristo
anawalazimisha wafanyakazi wetu wasio Wakristu waikane dini yao na kuwa
Wakristo. Alilenga kuibua chuki dhidi ya Waislamu na familia yangu.
Kwa hakika, mikakati hii ya kuichafua familia yangu
inasababishwa na harakati za ubunge Moshi Vijijini 2015. Wapinzani wangu
wanajua wazi kuwa hawana hoja ya msingi ya kuwafanya wapiga kura
wasinirudishe kwenye nafasi ya ubunge. Kwenye jukwaa na hata kwenye
medani ya maendeleo wanakwama. Kwa mfano, kabla ya barabara za lami
kuanza kujengwa walisema mimi sina ushawishi wa kuifanya Serikali
kuzijenga. Sasa zimejengwa na zinaendelea kujengwa wanajenga hoja kuwa
sihusiki wala Serikali ya CCM haihusiki, bali ni Benki ya Dunia
inajenga!!! Wananchi wanawauliza kwani kabla ya Dr Chami kuwa mbunge
Benki ya Dunia haikuwepo? Wanakosa hoja! Hivyo hivyo kwa mashule, maji,
vyuo vya ufundi nk.
Kwa hiyo kwa upeo wao wanaona silaha pekee waliyo nayo ni
kuzua kashfa dhidi yangu. Miezi michache iliyopita walizua nimeuza
shamba la KNCU kwa shilingi bilioni 4 wakati mimi sina wadhifa wowote
KNCU. Eti nimeuza nyumba mbili za Coffee Curing Moshi wakati mimi sina
wadhifa wowote Coffee Curing. Walipoona tuhuma hizo za kutunga hazijakubalika masikioni
mwa wapiga kura wa Moshi Vijijini, sasa wamezua hili la mke wangu kuua
ili Waislamu wa Moshi Vijijini wanione mtu nisiyefaa.
Sasa mimi napenda kuwauliza maswali haya:
Huyo
mke wangu muuaji anaitwa nani? Inaingia akilini kweli
kwamba mke huyo muuaji hafahamiki jina kwa hao "majirani" wetu wa
kufikirika? Binti Mariamu kauawa mji upi? Kwa nini majirani hao wenye
uchungu hawajatoa taarifa kwa RPC wa mkoa au kanda husika? Maiti
kahifadhiwa hospitali ipi? Au "mke" wangu amekaa naye ndani baada ya
kumuua na majirani wamekaa kimya tu?
Kwa desturi za dini ya Kiislamu binti huyo angeshazikwa
sasa maana kwa mujibu wa habari hiyo ya kizushi, "aliuawa" usiku wa
kuamkia jana. Je, kazikwa makaburi yapi na yako mji gani? Nani
kahudhuria hayo mazishi? Kwa nini vyombo vya habari visituonyeshe hayo
mazishi? Kwa nini RPC mhusika asimkamate huyo mke wa mbunge fedhuli namna hiyo na muuaji asiyevumilika?
Kwa nini polisi hawajaniita mimi Dr Chami kunihoji kuhusu
huyo "mke" wangu? Si wanajua niko jimboni Moshi Vijijini na RPC Boaz wa
Kilimanjaro anafahamu niko jimboni, tena jana nimeutembelea msikiti
mmoja kwa minajili ya kuutafutia umeme na maji? Sote tunafahamu kuwa kuna mkuu mmoja wa mkoa alimuua mtu
kwa kumpiga risasi na alikamatwa akapelekwa mahabusu. Huyo mke wa Dr
Chami ni maarufu kuliko Mkuu wa Mkoa? Kwa nini asikamatwe tuione sura
yake magazetini?
Majibu ya maswali haya HAYAPO kwa sababu kila kitu
kimetungwa kwa kujenga chuki tu. Hakuna Mariamu, hakuna kipigo, hakuna
kifo. Ila kuna UBUNGE WA MOSHI VIJIJINI. Ndio unaopiganiwa, hamna
kingine. Napenda kuwaasa wanasiasa wenzangu kuwa Watanzania wa leo
si wa jana. Si jambo rahisi kuwaghilibu kwa staili hii. Waende kwa
wananchi wachape kazi. Wasipofanya hayo wakadhani uongo wa mitandao
utawapa ubunge watashangazwa mwaka kesho 2015.
Mimi naendelea kuwaahidi wapiga kura wangu utumishi wa
dhati. Nawapa pole ndugu zangu wa Kiislamu kwa usumbufu walioupata.
Waislamu wa Moshi Vijijini wananifahamu kama kiongozi nisiyewabagua kwa
sababu ya dini yao. Wanafahamu kuwa nawapenda na nafahamu kuwa
wananipenda sana. Ndiyo maana wengi wamejiuliza iweje tena mke wangu
amwage damu ya Mwislamu kwa sababu iliyotajwa. Naendelea kuwaahidi
Waislamu wote upendo na ushirikiano siku zangu zote za kuwatumikia.
Wasalaam
Dr Chami.
DR.CHAMI KAMA HILO JAMBO SI KWELI KWA NINI USIFUATE SHERIA KWA KURIPOTI SUALA HILO KWENYE VYOMBO HUSIKA NA PIA KUDAI FIDIA KWA KUCHAFULIWA JINA LAKO NA HADHI YAKO.
ReplyDeleteVYOMBO VYETU VYA HABARI VINGI SANA HAVIFUATI MAADILI YA KAZI YAO. KWA NINI WASIKUAFUTE WAKAPATA UPANDE WA PILI WA SARAFU KULIKO KUANDIKA NA KUTAPAKAZA UCHAFU HUO.