Timu ya Riadha ya Mkoa wa Tabora ikiwa kwenye mazoezi makali katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ikijiandaa kushiriki mashindano ya riadha taifa yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii jijini Dar.
Na Allan Ntana,Tabora
TIMU ya Riadha ya mkoa wa Tabora ipo katika mazoezi makali kujiandaa na mashindano ya Riadha Taifa yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki hii jijini Dar e s salaam.
Katibu wa chama hicho Mkoa wa Tabora Salum Tarraddady, alisema jumla ya wanariadha 15 wa kike 9 na wa kiume 6 wapo kambini wakijifua kwenye uwanja wa Ali Hassan kujiandaa na mashindano hayo.
Alisema vijana wake wapo katika hali nzuri na wana ari kubwa ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo huku akiahidi kuuletea sifa mkoa wa Tabora kwa kunyakua medali nyingi.
“Vijana wetu wapo vizuri sana wakijiandaa na mashindano hayo ya kitaifa na wameahidi hawatawaangusha wananchi na wapenzi wa mchezo huo wa Tabora”Alisema.
Alibainisha kwamba wanafanya mazoezi asubuhi, mchana na jioni kila siku katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mratibu wa Riadha Mkoa wa Tabora, Allan Ntana, alisema wanamichezo wa Tabora katika mashindano hayo watashiriki mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1,500, 3,000, 5,000 na 10,000 ikiwemo mbio za kupokezana vijiti (relay) huku michezo mingine ikiwa ni kuruka chini na juu, miruko mitatu, kurusha mkuki, kisahani na tufe.
Ntana ambaye pia ni Afisa Habari wa Chama cha Riadha Mkoa wa Tabora, alisema vijana hao wamedhamiria kufanya vizuri zaidi tofauti na walivyofanya mwaka jana katika mashindano hayo kwani walirudi na medali zipatazo 10 zikiwemo dhahabu, fedha 3 na Shaba.
Alitoa wito kwa uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Tabora na wadau wengine wa michezo kuisaidia timu hiyo kifedha ili kufanikisha gharama za kuipeleka jijini Dar es salaam kushiriki mashindano hayo.
"Kila kitu kikienda kama tulivyopanga, tuna uhakika vijana wetu kutuwakilisha vema kama walivyotuwakilisha mwaka jana"Alisema.
Mambo yakienda vizuri timu hiyo inatarajia kuondoka Mkoani Tabora Alhamisi wiki hii ikiwa na Viongozi wawili pamoja na wanamichezo 15.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...