Mkurugenzi Sera na Utafiti wa TRA Bw. Tonedeus Muganyizi akizungumza na wana umoja wa uingizaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki zinazotoka nchi za nje wakati wa kikao cha wafanyabiashara hao na asasi zinazosimamia usambazaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki jana jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakijadiliana wakati wa kikao cha wafanyabiashara na asasi zinazosimamia usambazaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki jana jijini Dar es Salaam.

Na Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikalini WHVUM 

 Mkurugenzi Sera na Utafiti kutoka TRA Bw. Tonedeus Muganyizi amevitaka vyombo vya udhibiti vya kiserikali kufanya kazi kwa pamoja na TRA katika kusimamia sheria na kanuni za usambazaji na uuzaji wa kazi za Filamu na muziki nchini.

Rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kilichowahusisha wafanyabiashara wanaosambaza kazi za filamu na muziki pamoja na wadau wanaohusika na usimamizi wa usambazaji wa kazi za filamu na muziki kutoka TRA, Bodi ya Filamu, BASATA, pamoja na COSOTA baada ya wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi yao kuhusiana na operesheni inayoendelea ya kukamata kazi za filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi zisizokuwa na haki miliki na stempu ya TRA.

Aidha Bw. Muganyizi amesema kuwa kazi yoyote ya filamu na muziki inapaswa kuwa na haki miliki kabla ya kusambazwa ili kuiwezesha TRA kutoa stempu kwa kazi hizo jambo ambalo limekuwa likikiukwa na wafanyabiashara wanaosambaza na kuuza kazi hizo hivyo kupelekea Serikali kuendesha operesheni ya kusaka kazi za filamu na muziki zisisokuwa na haki miliki na stempu kutoka TRA.

Akitoa mchango wake Katibu Mtendaji kutoka Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo amewataka wafanyabiashara wa kusambaza na kuuza kazi za filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi na za hapa nchini kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kuweza kulinda mali zao na kufanya biashara kwa amani.

Bibi. Fisoo amesema kuwa kifungu cha 19, 1 cha sheria ya haki miliki ya mwaka 1996 kimefafanua kuwa uuzaji, usambazaji, ukodishaji na uonyeshaji wa filamu za picha jongevu uzingatie usajili kutoka Bodi ya Filamu kuziwezesha kazi hizo kuwa halali zinaposambazwa.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu kutoka COSOTA Bibi. Doris Antony amewataka wafanyabiashara kuheshimu haki miliki za wasanii kwani mmiliki wa kazi ya filamu na muziki ana haki 9 ambapo kati ya haki hizo tisa ni pamoja na haki ya kusambaza kazi yake, haki ya kuzalisha, haki ya kutafsiri, haki ya kuonyesha kwa Umma, haki ya kupeleka kwenye vyombo vya habari pamoja na haki ya kupeleka nje ya nchi.

Wakitoa mchango wao, wanaumoja wa uingizaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi wameiomba serikali kuwapa nafasi kumalizia mzigo uliopo sokoni kwa madai kuwa hawakuwa na ufahamu wa sheria inayosimamia haki miliki kitu ambacho serikali imekipinga na kuwataka kufuatilia haki miliki ya kazi walizonazo kwa wamiliki kuiwezesha serikali kutoa stempu zitakazowawezesha kuuza kazi hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...