Jana tarehe 16/07/2014 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ilifanya kikao cha kawaida cha siku moja mjini Dar es salaam. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa upande wa pili.

Mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi yana lengo la kuangalia kwa kina ni kwa nini baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba walisusia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo, na kuangalia namna watakavyorudi ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini.

Kwa ujumla Kamati Kuu ya CCM imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo na kupongeza juhudi hizo zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa na Vyama husika. Kamati Kuu inapenda kueleza imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda kwa wajumbe wachache waliosusia Bunge Maalum la Katiba, kurejea Bungeni na kumalizia sehemu ya mchakato uliobakia. Kamati Kuu inayatakia kila la kheri mazungumzo hayo.

Kamati Kuu pia ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais. Baada ya kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea, ni muhimu wakazingatia Katiba, Kanuni na taratibu za Chama zinazosimamia masuala hayo.

Kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za Chama kwa suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya mwenendo wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo mwezi wa nane (Agosti 2014), na kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati Kuu kuongezwa kwa adhabu kufuatana taratibu za Chama.

Ni muhimu wanachama wote wakakumbuka kuwa Chama ni pamoja na Katiba, Kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga, jambo ambalo halivumiliki.

Nia ya CCM kusimamia haya ni kuhakikisha Chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu sana, hasa tunapoelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Aidha, Kamati Kuu imewatakia kheri na fanaka Watanzania wote wakati huu wanapomalizia mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Imetolewa na:-

Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
17/07/2014

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...