Ujumbe wa Tanzania uliopo nchini Canada kwa ziara ya mafunzo ukiongozwa na Naibu Waziri Nishati na Madini, Charles Kitwanga (aliyenyoosha mkono), ukiwa katika chumba cha kusimamia mitambo ya kuzalisha methano (haionekani pichani) katika kiwanda cha kuzalisha malighafi hiyo kilicho katika jimbo la Alberta nchini Canada.
Ujumbe wa Tanzania uliopo nchini Canada ukiongozwa na Naibu Waziri Nishati na Madini, Charles Kitwanga (wa nne kutoka kushoto, waliosimama), ukiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa kampuni ya kimataifa ya kuzalisha na kusafirisha methano ya nchini Canada mara baada ya kufanya ziara ya mafunzo katika kiwanda hicho. Wengine katika picha ni Naibu Waziri, TAMISEMI, Kassim Majaliwa, (wa nne kutoka kulia, waliosimama). Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Ummy Mwalimu, (wa pili kutoka kulia waliosimama) pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Kampuni ya kimataifa inayotengeneza na kusafirisha malighafi methano ya nchini Canada  ‘Methanex’ imeeleza Kuwa Tanzania ni moja ya maeneo muhimu duniani yanayofaa kwa uwekezaji wa viwanda vya kutengeneza malighafi hiyo ambayo inatumika    kuzalisha kemikali mbalimbali kutokana na uwepo wa  hazina kubwa ya gesi asilia.

Hayo yamesemwa na Bw.Kevin Handerson, Makamu wa Rais wa kampuni ya Methanex kwa upande wa Amerika Kaskazini wakati alipokuwa akizungumza na ujumbe wa  Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga uliofika katika kiwanda cha kuzalisha methano kilicho katika  jimbo la Alberta nchini Canada ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo  kuhusu  usimamizi na uendelezaji wa tasnia ya uziduaji.

 Bw.Handerson ameeleza kuwa uzalishaji wa methano  utakuwa na  manufaa makubwa kwa Tanzania   kutokana na malighafi hiyo kutumika  katika masuala mbalimbali ikiwemo kutengeneza vifaa  vya plastiki, gesi inayotumika majumbani, kutumika kwenye vyombo vya usafiri, viwanda vya kutengeneza rangi,  viwanda vya mbao, kuzalisha umeme, kusafishia maji n.k

" Pamoja  na Tanzania Kuwa ni eneo muhimu kwa uwekezaji wa viwanda hivi vya kuzalisha methano ni muhimu Serikali ikatenga    eneo maalum  kwa ajili ya uwekezaji wa namna hii, na kuzingatia uwepo wa sera,  sheria, kanuni  madhubuti zinazoongoza sekta hii, pia kuwe na miundombinu imara ya usafirishaji, maji, umeme wa uhakika pamoja na uwepo wa  rasilimali watu". Alisema Bw. Handerson

Akieleza kuhusu uwezo wa kampuni hiyo,  Makamu Rais wa Methanex amesema kuwa, kampuni hiyo  ina uwezo wa kuzalisha  tani milioni 8.5 za methano kwa mwaka  na   husafirisha  malighafi  hiyo  katika  sehemu mbalimbali duniani ikiwamo  Hongkong, Shanghai, Beijing, Seoul, Tokyo, na Brussels.


 Vilevile Bw. Handerson ameeleza kuwa kampuni hiyo ya Methanex ipo  tayari kuja  kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa wanauzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika uwekekezaji wa viwanda hivyo, wana mfumo mzuri wa kutoa mafunzo kwa wazawa ili kushiriki katika miradi ya methano, vilevile wako tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kuendeleza  rasilimali hiyo kwa manufaa ya wananchi.

Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga  aliikaribisha kampuni hiyo kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa kuna kiasi kikubwa cha gesi asilia cha zaidi ya futi za ujazo trilioni  50 ambacho pamoja na kutumika kuzalisha umeme pia inaweza kutumika  kwa shughuli nyingine za kiuchumi ikiwamo kutengeneza methano na mbolea.

Alisema kuwa kuwa serikali  ya Tanzania  inakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta za Nishati na Madini ili kuleta maendeleo endelevu ya sekta hizo na kwamba zipo   sera, sheria na kanuni nzuri ambazo pamoja na mambo mengine zinalenga kuvutia  uwekezaji katika tasnia hiyo.

Katika Ziara hiyo ya Mafunzo, Naibu Waziri Kitwanga ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu  ya Bunge ya Nishati na Madini, Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira,  Ummy Mwalimu na Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ( TAMISEMI), Kassim Majaliwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...