Na Profesa Joseph Mbele
Wapenzi wa vitabu wakishajipatia nakala ya kitabu cha mwandishi fulani, huguswa pale mwandishi anaposaini kitabu hicho. Aghalabu mwandishi huandika ujumbe mfupi kwa mteja huyu na kasha kuweka sahihi. Ni jambo linalowagusa sana wasomaji. Mimi mwenyewe, kama mwandishi, nimeshasaini vitabu vyangu vingi. Ninazo baadhi ya picha za matukio haya kutoka miaka iliyopita.
Msomaji makini na mwanablogu Christian Bwaya hivi karibuni ameelezea vizuri katika blogu yake, hisia zake baada ya kujipatia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differencesambacho nilikuwa nimekisaini:
Namshukuru kwa dhati mwandishi wa kitabu hiki, Prof. Mbele kwa kunitumia kitabu hiki bila malipo, tena kwa gharama zake. Si jambo linalowatokea wengi. Ni furaha iliyoje hatimaye nimekipokea leo asubuhi. Naanza kukisoma kitabu hiki kwa mara nyingine, safari hii kikiwa na saini ya mwandishi. Ni upendeleo na muujiza wa pekee kunitokea katika siku za hivi karibuni. Ni lazima nimshukuru kwa dhati. Asante sana Profesa

Utamaduni wa kusaini na kusainiwa vitabu nimeuzoea. Hata juzi tarehe 2 Agosti, niliposhiriki tamasha la Afrifest kule Brooklyn Park, Minnesota, nikiwa na vitabu vyangu, wadau kadhaa walionunua vitabu vyangu waliomba kusainiwa.



Hapa anaonekana mdau akiniangalia wakati nasaini nakala yaMatengo Folktales, ambayo alikuwa amenunua hapo. Baada ya kusainiwa nakala yake, aliona furaha ya ziada kupiga picha nami huku akiwa ameshika kitabu hicho. Hiyo nayo ni kawaida hapa Marekani; wadau wakishanunua kitabu na kusainiwa, wanapenda kupiga picha na mwandishi, ikiwezekana.



Mdau huyu, aitwaye Adrian, m-Marekani Mweusi, alinifahamu tangu miaka kadhaa iliyopita. Alikuwa anasoma katika chuo fulani mjini Minneapolis. Kulikuwa na mkutano wa kitaaluma, nami nilikuwa mmoja wa wanajopo, nikitoa mada. Adrian alivutiwa sana. 

Halafu, alinisikiliza tena mwaka jana, nilipokuwa naongea katika jopo la watu wawili, nikiwa na Profesa Mahmud el-Khati, m-Marekani Mweusi, tukiongelea mbele ya umati, mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi.
Adrian ni msomi kijana makini. Tayari naona nyota yake imeanza kung'ara katika medani ya uongozi katika jamii. Nina imani atafika mbali katika jamii ya wa-Marekani weusi na Marekani kwa ujumla.


Hapa kushoto ni picha nyingine, kutoka hiyo hiyo juzi katika tamasha la Afrifest, nikiwa na mdau kutoka Liberia, ambaye alikuwa amenunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nami nikiwa nimekisaini. Inaonekana aliguswa sana, na hakuweza kujizuia kuniwekea mkono wake begani pangu.

Suala hili la kusaini au kusainiwa vitabu linastahili  kutafakariwa. Naamini lina vipengele kadhaa muhimu, kama vile kiutamaduni, kisoshiolojia, kisaikolojia, na kifalsafa. hata katika maduka ya vitabu hapa Marekani, aghalabu utaona vimepangwa vitabu vya mwandishi vikiwa na ujumbe "Signed copy." Jambo hili linaisukuma akili yangu kutaka kulielewa zaidi. Ningependa kujifunza zaidi kuhusu suala hili, kwa kusoma maandishi mbali mbali na kufanya tafakari mwenyewe.

You might also like:

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. HALAFU HUYO M-MAREKANI MWEUSI UNAFANANA NAE PROF. HAIKOSI TUKICHECK DNA YAKE ANAWEZA KUWA BABU WA MABABU ZAKE WALIKUWA WATANZANIA.TEHE TEHE TEHE TEHE TEHE.

    ReplyDelete
  2. Mdau wa kwanza umenena.

    Ni Mipaka ya Mataifa tu tunabaki kuwa sisi sote ni ndugu!

    ReplyDelete
  3. Prof. Mbele,

    Hongera sana kwa kazi kubwa ktk Suala la Uandishi wa Vitabu ila jukumu lipo huku nyumbani Tanzania ambako wajinga ni wengi saana kuliko werevu (KAMA TULIVYO ONA HAPO SIKU ZA NYUMA WAJINGA WAKIDHARAU JITIHADA ZAKO HUMU JAMVINI).

    Wengi wa Watanzania hawana Utamaduni wa kusoma Vitabu na Magazeti ukiona wanasoma Vitabu na Magazeti ni Vijarida vya budrudani na Magazeti ya Udakua na Michezo (KAMWE HAWASOMI ILI KUPATA UELEWA), hawana ujasiri wa kuuliza na kudadisi ili waelewe, wao hujichukulia kila kitu wanajua.

    Kwa wengi wa Watanzania huchukulia kusoma kama kupoteza muda na wengi hutumia Muda mwingi kuzungumzia watu wengine, kupeleleza wengine, majungu na usengenyaji, wala hawasomi ili kuelimika na mabishano yasiyo na akili kwenye Vijiwe!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...