Ushirikishaji wa wananchi nguzo ya kutekeleza BRN

TAASISI za Serikali zinazohusika katika utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) zimetakiwa kuhakikisha kuwa wananchi wanaelezwa mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Mpango huo.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo Jumatano na Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais-Usimamizi wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia utekelezaji wa BRN, Bw. Omari Issa alipokuwa akifungua Mkutano wa Kwanza wa Watendaji wa Serikali Kutathmini Utekelezaji wa BRN.

BRN ilianza kutekelezwa Julai mwaka jana ikisimamiwa na Kitengo kipya cha Rais kinachoshughulikia Usimamizi wa Miradi (PDB).

Akifungua mkutano huo uliohusisha Wakurugenzi wa Wizara zinazohusika na BRN na taasisi zingine za utekelezaji, Bw. Issa alisema kuwa katika mwaka mmoja uliopita BRN imeweza kuleta mageuzi makubwa katika utendaji na utekelezaji wa miradi.

Hata hivyo alisema mafanikio hayo na changamoto zake vinapaswa kuelezwa kwa umma ili kuwashirikisha wananchi wafahamu na kutoa mchango wao.

"Natoa rai kwa Wizara na taasisi zinazohusika na utekelezaji wa BRN kuimarisha mawasiliano kwa umma ili wananchi wawe na taarifa na pia tuweze kupata mrejesho wa kuwahudumia zaidi siku zijazo," alisisitiza Bw. Omari akifafanua kuwa PDB iko tayari kufanyakazi na Wizara kusaidia mawasiliano.

Akizungumzia mwaka mmoja wa utekelezaji wa BRN, Bw. Issa alisema moja ya mafanikio ni BRN kuimarisha ari ya watendaji wa Serikali katika kila mmoja kufanya maamuzi na utekelezaji wa haraka unaojali muda na matokeo.

"Wizara ya Maji ni moja ya mfano mzuri wa taasisi za Serikali ambako dhana ya BRN imeonekana kuleta mafanikio. Tulipoanza tu kutekeleza miradi ya kupeleka maji vijijini wataalamu waliokuwa makao makuu ya Wizara walihamishiwa mikoani na baadhi ya taratibu za manunuzi zikapunguzwa.

"Leo ninayofuraha kuwaeleza kuwa mfumo huu wa nidhamu ya utekelezaji wa BRN umefanyakazi kubwa. Katika wizara hiyo zaidi ya wananchi milioni mbili wamepatiwa maji vijijini ndani ya mwaka mmoja ikilinganishwa na idadi ya watu 500,000 (laki tano) tu waliokuwa wakipatiwa maji kwa mwaka kabla ya mfumo wa BRN kuanza," alisema.

Katika mkutano huo wa tathmini, watendaji hao wa Serikali watatumia muda huo kuchambua changamoto zilizoikabili BRN katika mwaka mmoja uliopita, kuainisha mikakati ya kushughulikia changamoto hizo na watendaji hao kuweka kiapo cha kujituma zaidi katika utekelezaji siku zijazo ili kupata matokeo makubwa zaidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...