Na Profesa Mbele



Leo nimepata zawadi ya kitabu, Picturing Hemingway's Michigankilichotungwa na Michael R. Federspiel. Kinahusu sehemu ya kaskazini ya jimbo la Michigan, ambapo familia ya Ernest Hemingway ilikuwa inakwenda kwa mapumziko. 

Kitabu kina picha na maelezo kuhusu sehemu hiyo, ambapo Hemingway alitembelea tena na tena wakati wa utoto na ujana wake. Hapa ni chimbuko la matukio ya riwaya ya mwanzo ya Hemingway,The Torrents of Spring na hadithi zake ziitwazo Nick Adams Stories. 







Nimeletewa kitabu hiki na Bwana David Cooper wa Ohio na mwanae Clay ambaye ni mwanafunzi wangu aliyekuja Tanzania mwezi Januari, 2013 katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa."

Baba huyu ndiye aliyetupeleka Montana kwa ndege yake mwaka jana,kuonana na Mzee Patrick Hemingway. Hapa kushoto ni picha tuliyopiga mjini Lakeville, Minnesota, kabla ya kuruka kwenda Montana. Bwana Cooper anaonekana kulia kabisa, halafu anafuata mwanae, halafu mwanafunzi wangu mwingine aliyekuwemo katika kozi ya "Hemingway in East Africa," na mimi naonekana kushoto kabisa.




Mwanafunzi aliyeniletea kitabu anaonekana nami pichani hapa kushoto, tukiwa kwenye mpaka baina ya hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

Nilipokipata kitabu hiki, yapata saa saba mchana, nilijawa na furaha, nikaanza kukisoma mara, lakini nikaona nipige kwanza simu kwa walioniletea. Nilimpata Bwana Cooper, nikamshukuru sana. Ameniambia kuwa yeye na mwanae walikiona kitabu hiki katika duka kule sehemu ya Michigan Kaskazini, wakaniwazia. Baada ya maongezi nimeendelea kukisoma, nikamaliza baada ya masaa mawili hivi.. 



Wameninunulia nakala yenye sahihi ya mwandishi, kama inavyoonekana hapa kushoto. (Ninaposema hivi, mawazo yangu yameshakwenda kwenye mazungumzo baina yangu na Ndugu Christian Bwaya kuhusu suala hili la kusainiwa vitabu).

Nilifahamu kuwa sehemu hii ya Michigan Kaskazini ni muhimu katika utoto na ujana wa Hemingway, lakini kitabu hiki kimenifungua macho zaidi kwa kuonyesha sehemu mbali kwa picha na maelezo. Picha nyingi ni za mtoto Hemingway na watoto wengine katika familia yao, picha za wanaukoo, na sehemu mbali mbali. Nyingi katika ya picha hizo sikuwa nimeziona kabla. Kwa yote hayo, nimefurahi sana.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Asante sana, Ankal Michuzi, kwa uamuzi wako wa kuuweka ujumbe wangu hapa katika blogu ya jamii, ambao niliuchapisha katika kiblogu changu cha Hapakwetu. Kwa namna hiyo, kama ulivyofanya siku zilizopita, umenisaidia kuusambaza sana ujumbe wangu.

    Nakushukuru pia kwa mambo mengine uliyonifanyia, miaka na miaka, kunisaidia katika juhudi zangu za kujijenga kama mwanablogu. Nimeona niseme hayo, kwani pamoja na ukimya wangu, nina shukrani tele moyoni. Mungu akubariki.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...