WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADU NI NA MICHEZO DKT FENELLA MUKANGARA |
Siku ya Vijana Duniani itafanyika tarehe 12 Agosti, 2014 ikiwa na lengo
la kuyafanya masuala mbalimbali ya vijana kutambulika katika jamii ya
Kimataifa. Mwaka huu, ujumbe ni “Vijana na Afya Kiakili”.
Tarehe
hii iliamuliwa kuwa Siku ya Vijana Duniani na Umoja wa Mataifa mwaka 1999. Hii
ni Siku maalum inayodhihirisha kutambua kazi muhimu zinazofanywa na vijana na
umuhimu wake katika jamii pamoja na kuwapa fursa kwa ajili ya kuongeza ufahamu
juu ya changamoto na matatizo yanayoukabili ulimwengu wa vijana.
Mijadala katika
maeneo maalum pamoja na taarifa juu ya kampeni mbalimbali zitafanyika katika
maeneo na nchi mbalimbali ulimwenguni kwa ajili ya kutoa hamasa kwa nchi
wanachama pamoja na jamii ili kuelewa mahitaji ya vijana, utekelzaji wa sera
mbalimbali katika kusaidia kupambana na changamoto zilizopo, pamoja na
kuwasaidia vijana kushiriki katika michakato ya utoaji wa maamuzi.
Siku ya Vijana Duniani ni kutambua na
kuthamini kuwa kipindi cha ujana kinaambatana na mabadiliko makubwa na ya
haraka na safari ya kutoka utotoni kufikia utu uzima inaweza kuwa ngumu na
yenye changamoto nyingi na hivyo kuhitaji utulivu na ukomavu wa akili. Kwa
Tanzania kijana ni mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 35.
Katika Siku hii na siku za mbeleni itakuwa fursa ya kuweza kutoa ufahamu
juu vikwazo mbalimbali vinavyowakabili vijana ikiwemo kunyanyapaliwa na
kubaguliwa, lakini pia kuwapa vijana nguvu ili waweze kutimiza malengo yao.
Tanzania kama sehemu ya duania inatambua na kuthamini changamoto maalum
zinazowakabili vijana walioko katika mazingira hatarishi pamoja na umuhimu wa
kuhakikisha kuwa wanahusishwa kikamilifu katika malengo ya maendeleo katika
ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na vijana pamoja na wadau wa
maendeleo ili kuunga mkono programu za elimu ya afya kwa vijana walioko ndani
na nje ya shule, walioko katika taasisi za mafunzo rasmi na zisizo rasmi ili
kukuza uwezo wa taarifa na mawasiliano ya kisasa.Katika ngazi ya kitaifa
Tanzania imedhamiria kukuza na kuboresha misingi ya kuwashirikisha vijana
katika maeneo ya sera mbalimbali, programu ya mikakati ya maendeleo ya vijana
ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika na kufanyiwa kazi.
Katika
kutekeleza eneo hili Tanzania inalenga kuweka fursa zitakazowawezesha vijana
kukuza utaalamu na ujuzi utakaowawezesha kufanikiwa katika kipindi cha mpito
kutoka ujana kwenda katika utu uzima kwa kuzingatia hali halisi ya mabadiliko
makubwa yanayoendelea kutokea duniani.Kwa kutambua umuhimu huu, Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inatumia fursa hii kuwakaribisha vjana
pamoja na wadau mbalimbali katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa ya mwaka
huu ambayo yatafanyika Mkoani Tabora kuanzia tarehe 08 – 14 Oktoba ikiwa ni
mwedelezo wa kuwapa vijana na wadau taarifa mbalimbali kuhusiana na maendeleo
kwa ujumla wake.
Tukiwa tunasherehekea Siku ya Vijana Duniani Wajibu wetu mkubwa ni kuona
kuwa vijana wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii
katika jamii wanazoishi.Katika Siku hii Vijana wote wanakaribishwa kuandaa
hadithi mbalimbali fupi zenye mafunzo, mashairi, picha mbalimbali, video na
kazi za sanaa ili kazi itakayoonekana inafaa iweze kuwa miongoni mwa kazi
zitakazojumuishwa katika Chapisho la Umoja wa Mataifa ‘Kuwajumuisha Vijana
Kijamii kwa kuzingatia Afya Kiakili’.
Imetolewa na wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...