Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda akitoa mada ya ufunguzi kwenye Mkutano wa Dunia kuhusu Amani na Usalama ulioanza leo (Agosti 10, 2014) jijini Seoul, Korea Kusini
 Mama Tunu Pinda akishiriki katika mjadala wa mkutano huo
Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda (wa nne kushoto) akiwa na watoa mada wenzake mara baada ya ufunguzi kwenye Mkutano wa Dunia kuhusu Amani na Usalama ulioanza leo (Agosti 10, 2014) jijini Seoul, Korea Kusini. Kutoka kulia ni mwana wa Mfalme wa kisiwa cha Maori kilichopo New Zealand, Whatumaona Paki; Mke wa Rais wa Fiji, Koila Nailatikau; Mke wa Rais wa visiwa vya Marshall, Bibi Lieom Anono Loeak, aliyekuwa Balozi wa UN katika Nchi zinazoendelea, Balozi Anwarul Chowdhury na Katibu Mkuu wa UPF, Bw. Tageldin Hamad.
 Picha ya pamoja baada ya ufunguzi.Picha zote na habari na Irene Bwire wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

MKE WA WAZIRI MKUU, Mama Tunu Pinda amesema wanawake wote duniani wanalilia amani na hawapendi vita wala machafuko kwani husababisha amani kutoweka kwenye familia na vifo vya watu wasio na hatia.

Ametoa wito huo leo mchana (Jumapili, Agosti 10, 2014) wakati akitoa mada kama mzungumzaji mkuu (keynote speaker) kwenye Mkutano wa Dunia wa siku tano ulioanza leo jijini Seoul, Korea Kusini.

Mkutano huo ambao umeandaliwa na taasisi ya Universal Peace Federation (UPF) ambayo inatoa ushauri kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uchumi na Kijamii unajadili masuala ya Amani, Usalama na Maendeleo.

Akiwasilisha mada yake kuhusu usalama, amani na maendeleo barani Afrika, Mama Tunu Pinda alisema: “Ninaiomba jamii ya Kimataifa duniani kote tusimamie amani na usalama kwani kinyume na hapo ni kuleta machafuko na vita. Wanawake hatupendi vita wala machafuko...,” alisema huku akishangiliwa.

Aliwataka washiriki wa mkutano huo wasimame katika nafasi zao kama baba na mama, kama kaka na dada na kuhakikisha kuwa dunia inakuwa ni mahali pazuri pa kuishi. “Ninawasihi tuendeleze maono ya Muumba wetu, tuweke utu mbele kwa kuwajali wengine na tuache kutanguliza maslahi yetu binafsi,” alisema.

Mapema, akiwakaribisha wajumbe zaidi ya 500 kutoka nchi 68 wanaoshiriki mkutano huo, Rais wa UPF, Dk. Thomas Walsh alisema taasisi hiyo inasimamia misingi ya amani, usalama na maendeleo ya jamii kwa nia ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa mataifa mbalimbali.

Alisema anatumaini uwepo wa wakuu wa nchi mbalimbali na viongozi mashuhuri, utasaidia kupata majibu ya changamoto inayoikabili dunia juu ya upatikanaji wa amani ya kudumu.

Naye, Mfalme Letsie Mswati III kutoka Lesotho, akizungumza katika mkutano huo alisema dunia inakabiliwa na changamoto nyingi za ukosefu wa amani kubwa ikiwa ni uharibifu wa mazingira. Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanahimiza utunzaji wa mazingira kama njia ya kupunguza matatizo yanayojikeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Alionya kwamba kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha kuwa dunia haiendelei kuwa na matukio ya kigaidi na matumizi ya silaha za maangamizi. “Kama tutakubali vita viendelee kutokea, na migogoro isiyokwisha barani Afrika na nchi za Uarabuni, ni lazima tukubali kuwa hakutakuwa na maendeleo katika mabara haya,” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...