Mkuu wa wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu (aliyeshika mkoba)
akikabidhi bajaj hiyo kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Vijana Simon
Mang’ombe.
Vijana walioko katika Kijiji cha Mafunzo Sikonge wakifurahia
chombo hicho cha usafiri kinachoendeshwa na kijana mwenzao.
Mmoja wa vijana wa Kijiji cha Mafunzo akitoa neno la shukrani
mbele ya mheshimiwa DC kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Bajaj iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa ‘Kijiji cha
Mafunzo ya Vijana’ wilayani Sikonge, mkoani Tabora.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Kayanza Peter
Pinda ametoa msaada wa bajaj kwa ‘Kijiji cha Mafunzo ya Vijana’
maarufu kwa jina la ‘Pathfinder Green City’ kilichoko wilayani Sikonge
mkoani Tabora.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mkuu wa wilaya ya
Sikonge Hanifa Selengu alisema bajaj hiyo imetolewa na mheshimiwa
Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji ahadi aliyotoa mapema mwaka jana
alipotembelea kituo hicho.
Alisema chombo hicho cha usafiri ni mkombozi kwa vijana walioko
kijijini hapo kwa kuwa kitawarahisishia ubebaji wa mazao na bidhaa
mbalimbali wanazozalisha kutoka eneo moja kwenda jingine hasa
ikizingatiwa kuwa ukubwa wa kijiji hicho ni takribani ekari 200 na
uzalishaji unafanyika katika maeneo mbalimbali ya kijiji.
Aliongeza kuwa chombo hicho kitatumika pia kubebea wagonjwa kutoka
kjijini hapo mpaka kwenye kituo cha afya mjini Sikonge, lakini
akawatahadharisha kutokitumia kinyume na utaratibu uliowekwa kwani
kufanya hivyo ni matumizi mabaya na kukiuka utaratibu jambo
litakalosababisha kiharibike mapema.
Serikali ya CCM inawajali sana vijana na inatambua umuhimu wao na
mchango wao katika uzalishaji mali ndio maana serikali imeruhusu
kijiji hicho cha kipekee cha mafunzo kwa vijana kianzishwe wilayani
humo sambamba na kutembelewa na wageni mbalimbali’aliongeza.
Akizungumzia utunzaji wa chombo hicho Selengu alisema uongozi wa
kijiji ndio utakaowajibika kukitunza sambamba na kupanga jinsi
kitakavyotumika katika shuguli mbalimbali za kijiji na sio za
kibinafsi huku akibainisha kuwa halmashauri ya wilaya ndiye mwangalizi
mkuu na itasimamia suala zima la matengenezo (servicing).
Aidha alisema kijiji hicho ambacho kinatoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali
kwa vijana wapatao 100 kwa nadharia na vitendo kimetenga maeneo
tofauti tofauti kwa ajili ya shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo cha
mazao mbalimbali, bustani (greenhouse), ufugaji wa kuku na ng’ombe,
ufyatuaji matofali, ujenzi na ufundi.
Baadhi ya vijana walioko kijijini hapo Said Salum, Tausi Jonas na
Simon Mang’ombe (Mwenyekiti wa kijiji) walimshukuru Waziri Mkuu
Mizengo Pinda kwa msaada huo kwani walikuwa wanapata shida sana
wanapotaka kusafirisha mazao na bidhaa zingine wanazozalisha toka
sehemu moja kwenda nyingine katika kijiji hicho.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Richard Unambwe ambaye pia
ni mwanasheria wa halmashauri hiyo aliwaasa vijana hao kukitumia
vizuri chombo hicho ili kiwasaidie katika mafunzo yao sambamba na
kutoa taarifa punde kinapoharibika.
Aidha Unambwe aliwahakikishia vijana hao kuwa halmashauri yake
itaendelea kutoa msaada unaostahili kijijini hapo ili kuhakikisha
malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa hususani kuwapa ujuzi mbalimbali
utakaowasaidia kujiajira wenyewe punde wamalizapo mafunzo yao kijijini
hapo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...