Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Jopo la majaji lililoundwa kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa tuzo ya Rais ya huduma
za jamii na uwezeshaji katika miradi ya madini, gesi na mafuta linatarajia kuanza kazi
yake kesho, imeelezwa.
Akizungumza katika kikao na majaji watakaoshiriki katika zoezi hilo kilichofanyika
kwenye ofisi za Wizara ya Nishati na Madini Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na
Madini Mhandisi Ngosi Mwihava amesema kuwa kazi hiyo inayotarajiwa kukamilika
Septemba 24, 2014 itahusisha mikoa yote ambayo miradi ya madini, gesi na mafuta
inaendesha shughuli zake.
Mhandisi Mwihava alisema lengo la zoezi hilo ni kushindanisha makampuni
yanayoendesha shughuli za madini, mafuta na gesi katika utoaji wa huduma bora kwa
jamii.
Alieleza kuwa mara baada ya jopo la majaji kumaliza kazi yake, litawasilisha ripoti
kamili ya zoezi hilo ambayo itadurusiwa kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa ajili ya
maandalizi ya halfa ya utoaji tuzo inayotarajiwa kufanyika mapema Novemba mwaka
huu.
“Tanzania imewaamini katika kazi hiyo, hivyo ni imani yangu kubwa mtatumia utaalamu
na uzoefu wenu katika zoezi hilo pasipo kupendelea kampuni yoyote. “ Alisisitiza
Mhandisi Mwihava.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Uunganishaji na Shirikishi Wadau katika Tasnia ya
Uziduaji (Extractive InterStakeholders Forum, EISF) Bi. Catherine Lyombe aliainisha
maeneo yatakayoangaliwa kama mchango wa makampuni yanayoendesha shughuli
za madini, gesi na mafuta kuwa ni pamoja na elimu, maji, afya, ajira na miundombinu.
Akielezea zoezi litakavyofanyika Bi. Lyombe alieleza kuwa majaji watatembelea
maeneo yote yenye makampuni yanayoendesha shughuli za madini, gesi na mafuta na
kuzungumza na wahusika pamoja na kuzungumza na wananchi ili kupata picha kamili
ya mchango wa makampuni husika kwa jamii.
Bi. Lyombe alisisitiza kuwa mbali na kupata taarifa kutoka katika makampuni na
maelezo kutoka kwa wananchi kama wataalamu watafanya ulinganisho wa maelezo
yanayotolewa na wananchi na tathmini halisi ya utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa
na kampuni husika.
Aliongeza kuwa lengo la utoaji wa tuzo hizo ni mkakati wa kuhamasisha makampuni ya
madini, mafuta na gesi kuboresha huduma zake kwa jamii.
“ Mshindi wa tuzo ya Rais ya huduma za jamii na uwezeshaji katika miradi ya madini,
mafuta na gesi anapopatikana, anatia hamasa kwa makampuni mengine kuboresha
huduma zake na wananchi kuendelea kunufaika na uwepo wa makampuni hayo”
alisisitiza Bi. Lyombe.
Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji (Presidential Award on Corporate
Responsibility and Empowerment –CSRE in Extractive Industry) katika miradi ya
madini, gesi na mafuta ilizinduliwa mwaka 2012 na Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
kama mkakati wa kuhamasisha makampuni ya madini, gesi na mafuta kuboresha
huduma zake kwa jamii hususan katika maeneo ya elimu, maji, miundombinu, ajira na
afya.
.jpg)
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ngosi Mwihava
akizungumza na jopo la majaji na sekretarieti inayotarajia kuanza kazi ya kumtafuta
mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji (Presidential Award on
Corporate Responsibility and Empowerment –CSRE in Extractive Industry).
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uunganishaji na Shirikishi Wadau katika Tasnia ya Uziduaji
(Extractive InterStakeholders Forum, EISF) Bi. Catherine Lyombe akielezea jinsi
zoezi la kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji
(Presidential Award on Corporate Responsibility and Empowerment –CSRE in
Extractive Industry) litakavyoendeshwa katika kikao hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...