Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mwezi wa Septemba, Muwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Balozi Samantha Power akizungumza wakati wa Mkutano wa Dharura wa Baraza Kuu la Usalama, uliofanyika Alhamisi kwa lengo la kukusanya nguvu za Jumuiya ya Kimataifa katika kuukabili mlipuko wa Ebola ambao sasa unaangaliwa katika jicho la kuwa tishio la amani na usalama wa Kimataifa.
Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama wakipiga kura ya kuunga mkono azimio namba 2177( 2014) kuhusu ugonjwa wa Ebola, azimio hilo linaelezwa kuwa huenda ndio likawa azimio la aina yake kupata uungwaji mkono mkubwa. Zaidi ya Mataifa 131 yameunga mkono azimio hilo ambalo linaweka mikakati ikiwamo ya vitendo na kisiasa ya kushughulikia mlipuko wa Ebola
Na Mwandishi Maalum, New York
Katika hali isiyokuwa ya kawaida katika historia ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa
ambalo limekasimiwa majukumu na dhamana ya masuala yote yanayohusiana na Amani na
Usalama wa Kimataifa, jana alhamisi limelazimika kukutana kwa dharura kujadiliana na kuweka
mikakati ya kuukabili mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na ambalo kwa mwezi huu wa Septemba lipo
chini ya Urais wa Marekani, lilikutana chini ya kichwa cha habari kilichosema “ Amani na
Usalama katika Afrika: Ebola”.
Kwa tafsiri ya haraka ni kuwa, Ugonjwa huo wa Ebola ambao umeshapoteza idadi kubwa ya
maisha ya watu katika nchi kadhaa za Afrika ya Magharibi kwamba, sasa siyo tu unachukuliwa
kama janga la kiafya, kibinadamu na kiuchumi bali umekuwa ni tishio kwa Amani na
Usalama wa Jumuiya ya Kimataita.
Ni kwa sababu hiyo basi, Jumuiya ya Kimataifa kwa maana ya Umoja wa Mataifa wenyewe
wanachama 193 imeamua kuuangalia kwa jicho pana zaidi mlipuko huo wa Ebola na
kuutafutia ufumbuzi.
Katika mkutano huo wa dharura na ambao kama ilivyoelezwa hapo juu uliandaliwa na Rais
wa Baraza hilo kwa mwezi huu (Marekani), licha ya kusikiliza hotuba au maelezo kutoka kwa
baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo akiwamo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataita, Mkurugenzi
Mkuu wa WHO na wawakilishi kutoka mataifa ambayo yameathiriwa na mlipoko huo,
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja Azimio namba 2177.
Azimio hilo ambalo limeungwa mkono na zaidi ya mataifa 131 ikiwamo Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania linaelezwa kama Azimio ambalo limepata uungwaji mkono mkubwa zaidi
pengine kuliko azimio lolote ambalo limewashi kuwasilishwa katika Baraza hilo.
Nchi ambazo hadi sasa zimeathirika kwa kiasi kikubwa na mlipuko huo wa Ebola ni Liberia,
Sierra Leone na Guinea. Zikiwamo Nigeria na nchi nyingine Cote d’ Ivoire na Senegal
ambazo nazo zimeeleza kukumbwa na mlipuko wa Ebola
Inaelezwa kuwa asilimia zaidi ya 50 ya wahanga wa mlipuko huo ni wanawake, ambao
kimsingi kutokana wa majukumu yao ndio walezi na watoa huduma ya kwanza kwa
wanafamilia wanaokumbwa na ugonjwa huo.
Katika mkutano huo wa dharura kila mjumbe aliyepata nafasi ukiacha wale waliotoa ahadi za
kutoa misaada ya hali na mali ikiwamo ya kibinadamu na fedha kwa nchi ambazo zimeathirika
na mlipuko huu, wametoa wito kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa na nchi zote bila ya kujali
ukubwa au udogo wake kuchukua hatua madhubuti za muda mfupi na muda mrefu kuukabili
mlipuko wa Ebola ambao hadi sasa hauna tiba.
Vile vile, wazungumzaji kadhaa wamezipongeza nchi ambazo zimekabiliwa na mlipuko huo kwa
hatua mbalimbali ambazo hadi sasa zimechukua katika kuukabili ugonjwa
Aidha baadhi ya wazungumzaji wamesisitia haja na umuhimu wa kutozitenga au kuzinyanyapaa
nchi ambazo zimeathirika kwa kile walichosema kinachotakiwa si kuzitenga bali kuzisaidia ili
kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huu hatari.
Mwakilishi wa Tanzania akichangia majadiliano hayo, alirejea ahadi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa hivi karibuni katika mkutano
wa Umoja wa Afrika uliofanyia Malabo, Equitoria Guinea kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana
kwa hali na mali na AU na washirika wengine katika kuukabili mlipuko wa Ebola.
Umoja wa Mataifa umekwenda mbali zaidi kwa kuanzisha Kituo cha Kwanza cha aina
yake kuratibu dharura ya Mlipuko wa Ebola na kuipandisha hadhi Misheni ya Kulinda
Amani nchini Liberia ili pamoja na mambo mengine iweze kuratibu na kusimamia misaada
inayohusiana na Mlipuko wa Ebola.
Katika kile kinachoonekana kwa Ebola ni tishio kwa amni na usalama , nchi kama vile
Marekani, Uingereza na Cuba na nyinginezo zenyewe zimeamua kuyahusisha majeshi yake
katika utoaji wa misaada, mafunzo na ujenzi wa vituo vya afya kama hatua ya kukabiliana na
Ebola.
Ni kweli Ebola si mchezo, ugonjwa unaotishia wanaougua, madaktari hata ndudu wanaouguza na waombolezaji unatisha.
ReplyDeleteHuyo Mzungu si Balozi Samantha Power; Samantha Power ni Mweusi!
ReplyDelete