Na Ali Othman Ali.
Mwandishi anayechipukia kwa kasi katika tasnia ya fasihi ya Kiswahili ambaye
pia ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu Cha London, SOAS na Cambridge
nchini Uingereza, Bwana Yussuf Shoka Hamad, hivi karibuni anatarajia kutoa
kitabu chake kipya na cha kwanza kuchapishwa kinachoitwa; ‘Paka wa Binti
Hatibu na Hadithi Nyingine’.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa simu kutoka nyumbani kwake jijini
London, Bwana Yussuf alisema; ‘ Msomi kama binadamu hufa, huzikwa na husahaulika
kama watu wengine wengi. Lakini msomi kama mwanataaluma na mwandishi hafi,
hazikwi, na wala hawezi kusahaulika kwani mawazo, fikra na falsafa zake hubakia
katika maandishi anayoyaacha. Na maaandishi hayo huwa ukumbusho na urithi
auachiyao jamii yake milele na milele.’
Bwana Yussuf pia alifafanua kwa upana kwanini ameamua kuandika kitabu chake kwa
kutumia lugha ya Kiswahili kwa kusema kwamba hadithi zilizomo humo zinawalenga
waswahili wenyewe na sio watu wa jamii nyengine. Kwa hivyo, sambamba na kukuza
na kukitangaza Kiswahili kimataifa, kitabu hicho kitatumika kuufiskisha ujumbe
uliokusudiwa kwa jamii kwa urahisi na kwa wepesi kwani lugha iliyotumika ni nyepesi na
yenye kufahamika kwa walengwa.
Alipoulizwa kwanini alichagua kukipa kitabu chake hicho jina la ‘Paka wa Bini Hatibu’
mwandishi alisema; ‘ Paka wa Binti Hatibu ni usemi uliozoeleka na wengi. Ingawa
kufahamika kwake kimaana na kimantiki kumekuwa kukileta mashaka yatokanayo
na bezo, kebehi na dharau, usemi huu unabaki kuwa na maana pana, tena zaidi ya
ile iliyozoeleka kimazowea ya kuukamilisha usemi wenyewe. Jina la Paka wa Binti
Hatibu, halimmuliki paka kama paka peke yake na Binti Hatibu kama tumjuavyo, bali
kinaimuilika jamii yote na wanajamii, wote kwa ujumla.’
Akitoa ufafanuzi kuhusu kitabu chake hicho ambacho utangulizi wake umeandikwa
na Mhadhiri wa masomo ya Fasihi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Bi Asha Khamis
Hamad, mwandishi huyo alisema kitabu chake kina hadithi saba na kila hadithi
kama kawaida yake ina ncha nyengine saba zinazoimulika jamii kwa undani na kwa
kina kipevu cha udadisi na upekuzi. Kila hadithi imebeba mikasa, vitimbi na viteweji
kedekede ambavyo kwa ujumla hutoa ujumbe na kuleta ladha ya ucheshi usio kikomo.
Akijibu suala la vipi na wapi aliuota ujuzi huo wa uandishi, mwandishi alisema kuwa.
Amekuwa akisoma kazi mbali mbali za waandishi, na pia ametembea sana na kusikia
mengi kutoka kwa magwiji wa simulizi na uandishi wakiwemo waandishi nguli katika
fasihi ya Kiswahili kama vile Professa Said Ahmed, Farouk Topan na Ali Mwalimu
Rashid ambao kwa pamoja walimpa moyo na ari ya kuandika.
Kitabu cha Paka wa Binti hatibu kinachapishwa na ‘The Jomo Kenyatta Foundation’
ya Nairobi nchini Kenya na kitatumika kama kitabu cha kiada katika masomo ya Fasihi
katika chuo kikuu cha London, SOAS nchini Uingereza mara tu baada ya kutoka hivi
karibuni.
Mbali na kitabu hiki, mwandishi huyu pia amekamilisha miswada mengine minne
ya riwaya na Hadithi fupi zinazosubiri kuchapishwa. Mwandihi hivi sasa anaandika
vitabu vya kitaaluma vya kufundishia Kiswahili shuleni na vitabu vitokanavyo na utafiti
wa mambo mbali mbali yahusuyo jamii na utamaduni wa watu wa Pemba. Moja ya
muswada wa kitabu kitokanacho na utafiti wake ni kile cha ‘Watu 40 Mashuhuri kutoka
Pemba’ ambacho utafiti wake unaendelea hivi sasa.
Mwandishi Yussuf Shoka Hamad (kulia) akiwa na Professa Said
Ahmed Muhamed alipomtembelea nyumbani kwake Limbani Wete hivi karibuni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...