
Mhe. Sitta ameyasema hayo leo Septemba
Mosi, 2014 katika mkutano wake na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya
Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) ambalo lilikuja katika Bunge Maalum
kwa lengo la kuwasilisha hoja zenye msisitizo kuhusu haki za watu wenye ulemavu
katika mchakato Katiba Mpya.
Mhe. Sitta amesema kuwa kazi
wanayoifanya ya kuyapokea makundi mbalimbali Bungeni hapo haina lengo la kuja
na hoja mpya na kuziwasilisha katika
Bunge hilo, bali ni mawasiliano ya kawaida yanayohusu safari kutoka Rasimu Mpya
ya Katiba mpaka kufikia katika Katiba Mpya inayopendekezwa ipatikane.
“Jambo lolote lililoandikwa na
binadamu halikosi kasoro, katika Rasimu hii ya Katiba tumegundua inayomapungufu
kadha wa kadha, kuna baadhi ya maoni ambayo hayakuzingatiwa ndiyo maana
tunayafanyia kazi ili yawemo katika Katiba Mpya itakayopatikana,”.alisema Mhe.
Sitta.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Inclusive Development Promoters and Consultants kutoka Dar es Salaam, Bw. Kaganzi Rutachwamagyo ambaye
pia ni mwanachama wa Shirikisho hilo,amesema kuwa Kikosi cha Ushauri kuhusu
masuala ya watu wenye Ulemavu kimeweka kipaumbele cha msisitizo wao ambao
unajielekeza katika hoja za kuongeza masuala ya mambo ya Muungano ambapo
wamependekeza kuwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kuongezewe suala moja
zaidi la Nane kwa mujibu wa Rasimu ya Pili ya Katiba ambalo ni uratibu wa
masuala ya haki, usawa na fursa na uwajibikaji kwa watu wenye ulemavu kama
jambo la Muungano.
Bw. Rutachwamagyo ameongeza kuwa hoja nyingine ya msisitizo
inahusiana na suala la uanzishwaji wa chombo cha uratibu wa haki, usawa wa
fursa na uwajibikaji wa haki za watu wenye ulemavu ambayo hii ni kwa mujibu wa
Ibara ya 33 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Mkataba
mwenza wa nyongeza iliyoridhiwa kwa pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na amesema kuwa wanataka chombo hiko kijulikane kama Tume ya Kitaifa Juu ya
Haki, Usawa wa Fursa na Uwajibikaji kwa Watu wenye Ulemavu.
Aidha, Bw. Rutachwamagyo amegusia pia juu ya hoja nyingine inayohusu
suala la Uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwenye Bunge la Tanzania, Baraza la
Wawakilishi, Mabaraza ya Madiwani utamkwe na Katiba na ukokotolewe kwa misingi
ya asilimia badala ya kuweka idadi mahsusi. “Mathalani, tunapendekeza kifungu 113
kisomeke kuwa asilimia 5% ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania watakuwa ni watu wenye ulemavu wakiwakilisha kundi hili na
watapatikana kwa kuchaguliwa na wahusika wenyewe,” alisema .
Aliongeza kuongeza kwa kuzitaja hoja
nyingine ikiwemo suala la matumizi ya lugha sanifu kwa muktadha wa watu wenye
ulemavu na amesema kuwa kuna hali ya matumizi ya misamiati na islahi ambazo
zinakinzana na dhana za walemavu kimataifa hivyo ni vema kukawa na tafsiri
sahihi ya majina kwa watu hao ili kuepuka kukinzana huko, aidha amegusia pia
suala la Hifadhi ya jamii huku akifafanua kuwa wadau wenye ulemavu nchini
wanadai kuwepo kwa ibara maalum ndani ya Katiba inayoelekeza masharti ya
upatikanaji wa hifadhi ya jamii kwa watu wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na
kulipwa gharama ama kupewa unafuu ya kupunguza makali ya walemavu kwa mujibu wa
ibara ya 28 ya Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu ya 2006.
Akiongea kwa niaba ya watu wenye
ulemavu, Mhe. Amon Mpanjo ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo amemuomba Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba kuunga mkono sio kupokea maoni mapya, bali
kuyaboresha yale yaliyokwisha wasilishwa hapo awali. “Tukuombe Mwenyekiti ulisisitizie
Bunge letu Maalum la Katiba liweze kuzingatia haki za watu wenye Ulemavu ili
nao wapate kuwa na maisha bora,” alisema Mpanjo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa SHIVYAWATA,
Bi. Amina Mollel amesisitiza juu ya hitaji la wanawake la hamsini kwa hamsini
na kati ya hizo, asilimia 5% wawe ni wabunge walemavu na ameitaka Tanzania kuwa
mfano wa kuigwa kwa kutoa nafasi nyingi za uongozi kada mbalimbali kwa walemavu. “Hii iwe chachu katika kuhakikisha
kuwa watu wenye ulemavu wanapewa nafasi kwa uwezo walionao na sio kubaguliwa,”
alisema Amina.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
01/09/2014.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...