Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuanzia mwezi ujao, Oktoba 2014, itaanza zoezi la kuvihakiki Vyama vya Kijamii hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine, zoezi hili linalenga kuvifuta kutoka katika daftari la Msajili vya Vyama vya Kijamii vyama ambavyo vitabainika kuwa havina sifa tena ya  kuendelea kuwa katika daftari hilo.

Vigezo ambavyo vinaweza kusababisha chama kufutwa kutoka katika Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii ni pamoja na kutolipa ada za mwaka kwa wakati na kutowasilisha kwa Msajili taarifa za kila mwaka za utendaji kazi na mapato na matumizi ya fedha za chama husika.  Kigezo kingine ni kwa chama kufanya shughuli tofauti na zile zilizoandikishwa katika katiba ya chama husika.
Ili kuvishirikisha vyama husika, Wizara wakati wa kuanza zoezi hili itachapisha katika baadhi ya magazeti majina ya vyama vyote vya kijamii vilivyopo katika kumbukumbu za daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii.
Baada ya kutangaza majina hayo, kila chama cha kijamii kitatakiwa kuhakikisha kuwa kimetekeleza matakwa ya kisheria yaliyobainishwa wakati wa usajili wa chama husika.
Baada ya  kipindi cha miezi mitatu tangu kutangazwa kwa tangazo hilo, Wizara itaanza kuchukua hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kukifuta katika daftari la Msajili chama cha kijamii ambacho kitakuwa hakijatekeleza matakwa hayo. 
Aidha, pamoja na mambo mengine, taarifa zitakazopatikana kutokana na zoezi hili la uhakiki pia zitawezesha kuanzishwa kwa database  ya vyama vya kijamii ambayo itasaidia kuboresha mawasiliano kati ya Msajili wa Vyama na vyama hivyo.
Hadi sasa Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii linaonyesha kuwepo kwa vyama vya kijamii 9,554 kote nchini. Kati ya hivyo, vyama vya kidini ni 956 na vyama vingine 8,598.
Jukumu la kusajili na kusimamia Vyama vya Kijamii linafanyika chini ya Sheria ya Vyama vya Kijamii SURA 337 (Societies Act Cap. 337) iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
Vyama vinavyosajiliwa chini ya Sheria hii ni pamoja na vyama vya kidini, vyama vya kitaaluma  na vyama vya maendeleo ya kijamii.

Imetolewa na:
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Pamoja na kuchapisha kwenye magazeti, ni vizuri pia kuweka orodha hiyo kwenye mtandao wa wizara.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...