Ajali za barabarani!
Ninalianza shairi, kwa majonzi ya dhahiri,
Kwa kuwa tena si siri, ajali zimekithiri,
Zaua kwa utitiri, hii sasa ni hatari,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Nianze na madereva, kisha nimvae Kova,
Unapokua dereva, tunahisi umeiva,
Si mambo ya kujilevya, na kuua kina Eva,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Umakini safarini, ndio nyenzo namba wani,
Sheria barabarani, zifuate kwa makini,
Sifa za vibarazani, hazina tija jamani!,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Bosi amekuamini, huyu “suka” ni makini,
Akakupa usukani, na vipesa kibindoni,
Vipi waweka rehani, roho za walio ndani?
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Ukanyagapo pedali, hakikisha unajali,
Roho za watu ni mali, kuzitoa ni muhali,
Japo unaenda mbali, mwendo kasi sio “dili”,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Nanyi wana usalama, sikizeni ‘nayosema,
Njiani mkisimama, fanyeni kazi kwa wema,
Adhabu kali lazima, hata kwa akina mama,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Rushwa nayo siyo njema, enyi wana usalama,
Kazi yenu ya heshima, na jukumu lenye dhima,
Ninawasihi kukoma, myafanyayo ni “noma”,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Na wale wenye magari, hili walitafakari,
Gari zataka vipuri, na madereva mahiri,
Gari mbovu sio nzuri, hata kwa walo hodari,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Naiomba serikali, hasa bwana Magufuli,
Njia zenye kona kali, ziboreshwe tafadhali,
Ziwe pana kweli kweli, tuzipunguze ajali,
Ajali barabarani, ni hasara kwa taifa.
Mwamgongo (Bw.)
Mwenyeji wa Tanga,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...