Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Wataalamu kutoka nchi za Zambia, Kenya na Tanzania kutoka Wizara
zinazoshughulika na masuala ya nishati wameanza majadiliano ya Utekelezaji wa
Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme katika Gridi za nchi hizo. Kikao cha
Majadiliano hayo kiliongozwa na Makatibu Wakuu kutoka katika nchi husika na
kitafuatiwa na mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 30 Septemba, 2014
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
Eliakim Maswi amezitaka nchi hizo kuunga mkono jitihada za utekelezaji wa
mradi huo kutokana na umuhimu wake kiuchumi ikiwemo kuhakikisha nchi hizo
zinakuwa na nishati ya umeme ya kutosha.
Aidha, ameongeza kuwa, tayari Tanzania imeanza kufanya jitihada mbalimbali
za kuhakikisha inaanza utekelezaji wa mradi huo ambao umechukua kipindi
kirefu kuanza kutekelezwa na kuongeza kuwa, Tanzania iko tayari kushiriki katika
utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kuhakikisha kwamba mradi huo unafanikiwa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Petroli Kenya
Mhandisi Richard Mwiru, ameeleza kuwa, kuna matokeo bora yatakayotokana
na utekelezaji wa mradi huo, matokeo ambayo yatasaidia biashara ya umeme na
upatikanaji wa umeme rahisi kwa nchi hizo. Aidha, ameongeza kuwa, nchi ya
Kenya iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Migodi,Nishati na Maendeleo ya Maji wa
Zambia, Charity Mwansa, ameeleza kuwa, anatarajia mkutano huo utatoa fursa
zitakazosaidia utekelezaji wa mradi huo kuendelea kutoka mahali ulipofikia
ili kuweza kutoa matokeo chanya yatakayokuwa na manufaa kwa nchi hizo
ukizingatiwa kuwa, nchi hizo zimebahatika kuwa na rasilimali asilia za kutosha.
Aidha, Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Soko la pamoja la nchi za Mashariki
na Kusini mwa Afrika anayeshughulikia miradi (COMESA), Dkt. Kipyego Cheluges
amezitaka nchi hizo kuhakikisha kwamba mradi huo unatekelezwa kutokana
na manufaa ambayo nchi hizo zitayapata ikiwemo bara la Afrika na kuongeza
kuwa, COMESA itashirikiana kwa karibu na nchi hizo kuhakikisha kwamba, mradi
unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, akiongea wakati
wa kikao cha Wataalamu kutoka nchi za Zambia, Kenya na Tanzania Kujadili
Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme katika Gridi za nchi
hizo. Wengine kutoka kushoto ni Balozi wa Zambia nchini Judith Kapijimpanga,
Katibu Mkuu Wizara ya Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji Zambia, Charity
Mwansa, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Petroli Kenya, Mhandisi
Richard Mwiru na Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Soko la pamoja la nchi za
Mashariki na Kusini mwa Afrika anayeshughulikia miradi (COMESA), Dkt. Kipyego
Cheluges.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Petroli Kenya, Mhandisi Richard
Mwiru (wa pili kulia) akiongea jambo wakati wa kikao hicho, ambapo ameeleza
utayari wa nchi ya Kenya katika utekelezaji wa mradi huo.
Sehemu ya Wataalamu kutoka nchi za Zambia, Kenya na Tanzania wakifuatilia
kikao cha Kujadili Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme
katika Gridi za nchi hizo.
Mtaalamu Mwelekezi kutoka nchi ya Zambia Siyanga Zomba, akiwasilisha taarifa
ya utekelezaji na hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa
kuunganisha Mtandao wa Umeme katika Gridi kwa nchi za Zambia, Kenya na
Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...