Sekretarieti ya CPA Kanda ya Afrika inasikitika
kutangaza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, (CPA) Dkt.
William Ferdinand Shija (pichani) kilichotokea katika Hospitali ya Charring Cross, London
Uingereza tarehe 4 Oktoba, 2014.
Taarifa ya kifo chake imekuja wakati
ambapo Mkutano wa 60 wa CPA unafanyika Yaoundé, Cameroon.
Dkt. William Shija amefanya kazi kwa
takriban miaka 8 kama Katibu Mkuu wa Chama cha Wabunge wa Jumuiya ya Madola.
Amefanya kazi kubwa kwa CPA na ameacha rekodi kubwa ya utendaji wa kazi akiwa
pia ndio Katibu Mkuu wa kwanza kutoka Afrika katika Chama hicho.
Katika uhai wake, Dkt. William Shija
amefanya kazi ikiwa ni pamoja na kushikilia nyadhifa zifuatazo katika Serikali
ya Tanzania:-
§ Waziri
wa Viwanda na Biashara;
§ Waziri
wa Nishati na Madini;
§ Waziri
wa Habari na Utangazaji
§ Waziri
wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu; na
§ Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza.
Aidha, Dkt. William Shija amekuwa
Mbunge kwa takriban miaka 15. Akiwa Mbunge, Dkt. William Shija alikuwa
Mwenyekiti na Mjumbe katika Kamati zifuatazo:-
§ Mambo
ya Nje; na
§ Habari;
Utamaduni na Utalii.
Vile vile, amewahi kuwa Mbunge wa
Bunge la Afrika ambapo aliongoza Timu ya Uangalizi wa Uchaguzi kutoka Bunge hilo
kwa Uchaguzi Mkuu wa Malawi mwaka 2004.
Kitaaluma, Dkt. Shija amesoma na
kuhitimu Shahada za Uzamili na Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Howard Nchini
Marekani. Alisoma na kuhitimu Shahada ya kwanza na Stashahada ya Uandishi
katika Chuo Kikuu cha New Delhi. Amefanya kazi kama Mhadhiri Mwandamizi katika
Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Nyegezi na pia amewahi kufundisha katika Chuo cha
Utumishi wa Umma na Chuo cha Uhazili Tabora.
Dkt. Shija ameacha Mke Bibi Getruda
Peter Shija na watoto watano; Leo, Anna, George, Ferdinand na Monica.
Sekretarieti ya CPA kwa kushirikiana
na Familia ya marehemu, Bunge la Tanzania, Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza
na Mwajiri wake CPA Makao Makuu na CPA Makao Makuu inaratibu mazishi yake
ambapo mwili wa marehemu utawasili nchini tarehe 11 Oktoba, 2014 na kuagwa
rasmi katika Viwanja vya Karimjee siku ya Jumapili tarehe 12 Oktoba, 2014 kabla
ya kusafirishwa kuelekea Sengerema kwa mazishi.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya
marehemu mahala pema peponi;
AMINA
Dkt. Thomas
Didimu Kashililah
KATIBU
WA CPA KANDA YA AFRIKA


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...