Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Halmashauri ya Geita  itaanza kupata  wastani wa  Dola za Marekani milioni 1.8 kwa mwaka  kutoka Mgodi wa  Dhahabu wa  Geita (GGM) baada ya kusainiwa rasmi kwa marekebisho ya mkataba  baina ya kampuni hiyo na Serikali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo  kabla ya kutiliana saini marekebisho ya mkataba huo  ambao uliosainiwa  awali mwaka 1999. Awali, Halmashauri hiyo ilikuwa ikipata  ushuru wa huduma wa  Dola za Marekani  200,000 kila mwaka badala ya kulipwa  asilimia 0.3 ya mapato ghafi ya kila mwaka  kama sheria ya fedha ya serikali za mitaa ya mwaka 1982 inavyotaka.

Kwa kuzingatia kiwango cha mapato ghafi  ya mgodi wa Geita kwa mwaka yanayopatikana hivi sasa,  Halmashauri ya Geita itakuwa na uhakika wa kupata  kiasi kisichopungua  Dola za Marekani  milioni 1.8 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa makubaliano  yaliyofikiwa  kati ya Serikali  na wamiliki wa mgodi huo, malipo hayo yataanza kulipwa  rasmi kuanzia tarehe 01 Julai, 2014.
Profesa Muhongo alisema kuwa fedha hizi ni nyingi mno  na kuwataka  wananchi wa Geita kujiandaa kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu  pamoja na huduma za jamii  zitakazopelekea uchumi wake kukua kwa kasi.

Profesa Muhongo alisisitiza kuwa ni vyema makabidhiano ya  fedha hizo kwa njia ya hundi yakafanyika kwa uwazi mbele  ya wananchi ili kupunguza malalamiko, ikiwa ni pamoja na kuongeza imani kati ya wananchi na migodi.

Aidha, aliwataka Viongozi wa Halmashauri hiyo,   kusimamia vyema fedha hizo kwa kuhakikisha kuwa zinachangia katika shughuli za maendeleo badala ya kutumika katika matumizi yasiyo ya lazima na tija katika jamii, hususani kulipana posho  za vikao na safari.

“ Kwa mazingira ya sasa, mji wa Geita hauna sababu ya kukosa maji, barabara bora, vituo  vya afya, ni imani yangu kuwa fedha hizi zitachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Geita iwapo zitasimamiwa ipasavyo,” alisema.

Maeneo mengine yaliyofanyiwa  marekebisho  kwenye mkataba wa awali  uliosainiwa mwaka 1999 ni kupandisha kiwango  cha malipo ya mrabaha kutoka asilimia  tatu ya mapato baada ya kuondoa gharama za uchakataji madini na kufikia asilimia nne ya mapato ghafi.

Eneo jingine lililofanyiwa marekebisho ni kufuta kipengele kilichokuwa kinatoa nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa. Kuendelea kuwepo kwa kipengele hiki kwenye mkataba, kungeipunguzia serikali  kodi ya mapato.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Tunashukuru wizara kurekebisha mikataba kwa manufaa ya nchi. Japo sijaulizwa ngoja niwasaidie wahusika kuorodhesha maeneo yanayoweza kutumiwa na fedha hizo. Tumieni fedha hizo kuendeleza na kubadilisha kabisa mji wa Geita Barabara za lami, miundo mbinu ya maji na usambazaji wa maji safi, hospitali na shule ziboreshwe, Uboreshaji wa kilimo utengewe fedha kuewe na trekta za kukodisha kwa bei nafuu. Stendi za basi za kisasa zenye pavement na viti zisizokuwa na vumbi, makazi ya kisasa kwenye sehemu zilizopangwa yajengwe kama mradi wa halmashauri kuzipangisha, ofisi, masoko,maduka, youth community centre zenye hall yenye tv and technical institute moja ijengwe kwa makudsudi hayo ya kutunisha mfuko wa mkoa. Nyumba duni ziondoshwe kwa kutoa small grants au mikopo nafuu kwa wananchi kuboresha nyumba zao, umeme, taa za barabarani za solar, Public toilets za kulipia za uhakika. Parking areas zinazolipiwa na kueleweka n.k. Mshindwe nyinyi tu kuzifanyia vitu vya maana vitakavyoneemesha jamii.

    ReplyDelete
  2. Wewe huijui Halmashauri ya mji wa Geita walikuwa wanapewa fedha na GGM kwa ajili ya Ujenzi wa Shule ya wasichana ya Nyankumbu hakuna kilichofanyika mpaka pale GGM walipoingilia kati kuanza kuijenga hiyo shule wao wenyewe.Natamani hizi hela Mhongo angezisimamia mwenyewe ila siyo kuwapa hao kupe wa H/Mashauri ya Geita

    ReplyDelete
  3. Wizara husika ifuatilie uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizi. Hatuwezi kuwa maadui wa maendeleo yetu wenyewe. Ikiwa hivyo sijui tusaidiweje, maendeleo yanawezekana viongoziwakiwa na maono, mikakati na wakijituma siyo tu kwa kusukuma mafaili bali maendeleo yanayoonekana. Siku zijazo kuwe na vigezo, mashindano kati ya Halmashauri za kanda na tuzo ili kuhimiza hatua za maendeleo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...