Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii kanda ya kaskazini.
WAKAZI wa kata ya Shirimatunda katika
maanispaa ya Moshi, wameingiwa na hofu ya kupoteza maisha yao,kufuatia
taarifa za kuwapo kwa mtu anayedhaniwa kuwa na ugonjwa hatari wa Ebola
anayehudumiwa katika zahanati ya kata hiyo.
Kutokana na hofu hiyo,halmashauri ya manispaa ya Moshi imelazimika
kuifunga kwa muda usiojulikana zahanati hiyo na kuwahamishia wagonjwa
katika hospitali nyingine ikiwamo ya St Joseph katika manispaa hiyo.
Ripota wetu ambaye alikuwa eneo la zahanati hiyo alishuhudia baadhi ya
madaktari wakiongozwa na mganga mkuu wa manispaa hiyo,Dk Christopher
Mtamakaya pamoja na wataalamu wengine wa afya wakifanya kikao cha
dharura kujadili hali hiyo.
Kadhalika,waandishi wa habari waliokuwepo katika zahanati hiyo
walishuhudia baadhi ya wataalamu wa afya wakiwa na mavazi rasmi
yanayotumiwa na madaktari wanaohudumiwa wagonjwa wa Ebola.
Pamoja na kikao hicho,Zahanati hiyo imewekwa tangazo katika lango kuu
linalosomeka 'Huduma zote za afya zimesitishwa kwa muda, Utawala' hali
ambayo imeendelea kuzua maswali mengi kwa wagonjwa wanaokwenda kupata
matibabu katika zahanati hiyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kigongoni,kata ya Shirimatunda ilipo zahanati
hiyo,Juma Sambeke alisema hajashirikishwa katika maamuzi ya kugeuza
Zahanati hiyo kama Karantini ya mtu anayedhaniwa kuwa na Ugonjwa wa
Ebola.
Alisema kuwapo kwa karantini hiyo kumeanza juzi majira ya saa 10 jioni
baada ya kupokea taarifa kutoka afisa mtendaji wa kata hiyo kwamba
zahanati hiyo itafungwa kwa muda ili kumhudumia mtu anayedhaniwa kuwa
Ebola.
"Manispaa haikuwa sahihi kuitumia zahanati hii kama karantini ya hofu
ya Ebola, hapa kuna shule ya chekechea, sekondari, seminari ya Don
Bosco na majirani kama unavyowaona....wasipopewa elimu na kama huu ni
ugonjwa wa Ebola watu watakufa sana"alisema.
Sambeke alisema maeneo yatakayoathirika zaidi na kufungwa kwa zahanati
hiyo ni Shirimgungani,Cherereni ya Moshi vijijini,Karanga,
Soweto,Bonite madukani na mtaa wa Kigongoni ambapo zahanati huudumia
zaidi ya watu 5,000 kwa mwezi.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Shirimatunda,Felix Mushi alisema
huduma za utoaji wa chanjo ya magonjwa ya Rubella na Surua
zimehamishiwa katika ofisi ya mtendaji wa kata hiyo huku wagonjwa
wengine wakihamishiwa maeneo mengine.
Alisema tarifa za awali alizopata ni kwamba mtu huyo alipokelewa
katika uwanja wa ndege wa kimataifa Kilimanjaro (KIA), ambapo
alisafirishwa hadi kwenye zahanati hiyo baada ya kudai kuwa na dalili
zinazoashiria ugonjwa wa Ebola.
Aidha taarifa zaidi zinadai kuwa wataalam wamechukua sampuli kutoka
kwa mgonjwa huyo kwa ajili ya vipimo, ili kujiridhisha, wakati huduma
nyingine za matibabu zikiendelea kutolewa kwa mgonjwa huyo anayedaiwa
kusafiri kutoka nchini Senegal.
Mmoja wa wakazi anayeishi jirani na zahanati hiyo, Thadei
Sangawe,alisema ameanza kufanya mawasiliano na ndugu wengine waliopo
maeneo mengine mkoani humo ili aweze kuhamisha familia yake kuepuka
madhara kama ugonjwa huo utakuwa wa Ebola.
"Tunaomba viongozi wenye dhamana hususani madaktari watoe taarifa kwa
wananchi juu ya hii hofu iliyopo,maana kukaa kwao kimya kutasababisha
wananchi washindwe kuchukua tahadhari na hivyo kusababisha
madhara"alisema.
Hata hivyo akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi wa manispaa
ya Moshi Shaban Mtarambe, alisema hayuko tayari kuzungumza kwa maelezo
kuwa suala hilo ni la kitaalam zaidi linalohitaji waataala wa kada ya
afya kulizungumzia.
Naye mganga mkuu wa manispaa ya Moshi,Dk Christopher Mtamakaya
alipohojiwa kuhusiana na taarifa za kuwapo kwa mgonjwa huyo hakuwa
tayari kuzungumza zaidi na alipotumiwa ujumbe wa simu ya mkononi
alijibu kwa kifupi, huo ni Uvumi.
Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa huo,Dk Mtumwa Mwako alipohojiwa
kuhusiana na kuwapo kwa mgonjwa huyo naye alisema hafahamu na aliomba
kupewa muda kwani alikuwa katika kikao.
Kuhusiana na suala la mgonjwa huyo,katibu tawala wa mkoa huo, Dk
Faisal Isa alisema taarifa za kwanza anapata kutoka kwa mwandishi wetu
na akaomba muda wa kufuatilia zaidi.
.jpg)

Baadhi ya wagonjwa na wauguzi katika zahanati ya Shirimatunda
wakihamia katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Shirimatunda kuendelea na huduma za tiba ikiwamo utoaji wa chanjo ya Surua na Rubella
wakihamia katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Shirimatunda kuendelea na huduma za tiba ikiwamo utoaji wa chanjo ya Surua na Rubella
Kaka Michuzi asante kwa hii post, please endelea kulifuatilia kwa maana kuna facts za ugonjwa na pia kuna protocol iwapo mtu atakumbwa na ugonjwa huo.
ReplyDeleteAwali ya yote tafadhali madaktari watoe elimu haraka sana kuondoa hofu ya ugonjwa huu. Pia familia ya mgonjwa ikiwa ni mgonjwa pamoja na yeyote aliyemhudumia na hasa kama ametapikia mahali, harishia sehemu au kama ametoka damu kama vile wagonjwa wa ebola NA kama mtu alisafisha moja au vyote AU kama mtu alitapikiwa, hariahiwa pasi hilo ndilo la kufuatilia.
kama ni homa na ni kali sana, siyo rahisi kuambukizwa wakati. Ebola inambukiza kama maji maji ya mwili wa mgonjwa yakigusana na wahudumu ama mtu aliyerukiwa.
Jamani madaktari toeni semina kwenye radio, internet, misikitini, kanisani, vijijini na sehemu za mihadhara kuelimisha watu ili wajipange sawa!
Asante Kaka kwa hi nafasi natunaomba wasihi madaktari watusaidi, nilochosema mimi nimetoa kwenye mtandao.