Na Ally Mataula,
Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Mrisho Mashaka Gambo leo amefikishwa mbele ya Baraza
la Maadili ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Akisoma hati ya malalamiko
yanayomkabili Mhe. Gambo, Mwanasheria wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Hassan Mayunga alisema kuwa
Mhe. Gambo amekuwa akitumia lugha ya matusi
na kashfa dhidi ya watumishi wa Halmashauri ya Mji Korogwe kinyume na Misingi ya Maadili ya
Viongozi kwa mujibu wa fungu la 6 la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma sura
(398).
Pia, Mhe. Gambo analalamikiwa kuwa
aliweka shinikizo kwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kukiuka Taratibu za
Manunuzi ya Umma kinyume na matakwa ya fungu la 6 (c ) linalomtaka Kiongozi wa
Umma kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria.
Aidha, lalamiko lingine linalomkabili
Mhe. Gambo ni kuweka shinikizo lisilofaa
kumuhamisha Mtumishi wa Umma kinyume na fungu la 12 (1) (c) la Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, sura 398.
Hata hivyo Mhe Gambo alikana
malalamiko yote yaliyowasilishwa mbele ya Baraza dhidi yake na Shauri lake limeahirishwa
mpaka tarehe 15 Oktoba, 2014 ambapo Baraza litapata fursa ya kusikiliza
ushahidi kutoka upande wa Mlalamikiwa baada ya leo kuanza kusikiliza ushahidi
kutoka upande wa Walalamikaji.
Awali Baraza la Maadili lilianza
kusikiliza shauri linalomkabili Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora
Bibi Sipora J. Liana ambaye wakati akifanya makosa alikuwa ni Mkurugenzi wa
Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Akisoma hati ya malalamiko,
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bibi Getrude
Cyriacus alisema kuwa Mlalamikiwa bila sababu za msingi na bila kufuata
utaratibu alimchukulia hatua za nidhamu kwa kumsimamisha kazi Dkt. Francis
Malya aliyekuwa Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Wilaya ya Mkuranga kinyume
na fungu la 12 (c) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995.
Bibi Cyriacus aliendelea kumsomea
malalamiko mengine Mlalamikiwa ambayo ni Mlalamikiwa bila kufuata taratibu
alifuta hoja za ukaguzi za robo ya nne ya mwaka 2009/2010 kwa kumuagiza
aliyekuwa mhasibu Bw. Shabani Yusuph kufanya hivyo kinyume na matakwa ya Sheria
ya Fedha ya 2004 pamoja na Mlalamikiwa kutumia wadhifa wake kujinufaisha
kinyume na fungu la 12 (1) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya
1995 kwa kukiuka taratibu za Manunuzi katika Serikali za Mitaa za mwaka 2007
kwa kutafuta yeye mwenyewe na kuwalipa fedha wazabuni ambao hawakupitishwa na
Bodi ya Zabuni.
Maelezo ya malalamiko yaliyosomwa na
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bibi Getrude
Cyriacus yalifuatiwa na kusikilizwa kwa ushahidi kutoka upande wa Walalamikaji
uliotolewa na Dkt. Francis Malya ambaye alilieleza Baraza la Maadili namna Bibi
Sipora Liana alivyoshiriki kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja
na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa umma na kutoa vielelezo mbalimbali
ili kuweza kulilidhisha Baraza hilo ukweli wa maelezo yake.
Hata hivyo Mlalamikiwa alikana tuhuma
zote dhidi yake na kuomba nafasi ya kuitwa mashahidi wake mbele ya Baraza ili
nao wapewe nafasi ya kutoa maelezo kuhusu shauri hilo ambapo Baraza hilo
lilimkubalia ombi lake na Shauri lake liliahirishwa mpaka tarehe
itakayotangazwa hapo baadae.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Msaidizi -
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bibi Sara Kinyamfura Barahomoka
amejisalimisha mbele ya Baraza la Maadili baada ya kutolewa agizo la kukamatwa
baada ya kukaidi wito wa kufika mbele ya Baraza tarehe 10 Oktoba, 2014 kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Hata hivyo Mwenyekiti wa
Baraza hilo Mhe. Jaji (Mst.) Hamis Msumi alimpa onyo kwa kosa hilo na
kuahirisha kusikiliza shauri lake mpaka tarehe 15 Oktoba, 2014 ambapo litaanza
kusikilizwa kwa mara ya kwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...