Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeahidi kuendelea kuzisaidia redio jamii kwa lengo la kuhakikisha sauti za wanyonge zinapazwa na kusikika ili kukuza demokrasia nchini.
Mwalikishi wa shirika hilo ambaye pia ni mshauri na mkufunzi wa redio jamii Bi Rose Haji Mwalimu aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Redio Jamii cha Uvinza FM kilichozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya.
Bi Haji alisema kwamba jitihada hizo ni kutokana na ukweli kwamba watu wengi wanaishi vijijini ambako hawapati fursa ya kupata habari kwa wepesi kwa ajili ya maendeleo yao kwa sababu wanaishi katika sehemu ambazo hazifikiki kwa urahisi kutokana ya miundombinu duni ya mawasiliano.
“Takwimu zinaonyesha kwamba nchini Tanzania watu wenye uwezo wa kuangalia telelvisheni ni asilimia 7 tu, kwa hiyo redio bado inachukua nafasi kubwa zaidi ya upatikanaji wa taarifa kwa haraka, wepesi, urahisi na kwa mapana zaidi,” alisema Bi. Rose Haji.
UNESCO ni shirika la Umoja wa Mataifa ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitoa msaada kwa redio jamii Tanzania katika kuzianzisha, kuzipatia vifaa na kuzijengea uwezo kiufundi na mafunzo ili zijiendeshe zenyewe.
Redio zilizoanzishwa na UNESCO ziko chini ya mtandao maalum ujulikanao kama Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA).
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akifanyiwa mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji wa kituo hicho, Kadisilaus Simon mara baada ya kuzindua rasmi redio hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...