Na Mwandishi Wetu

MWANAMICHEZO maarufu nchini, Azim Dewji amewataka wanachama na wapenzi wa timu ya soka ya Simba kuamini timu yao bado ni bora, isipokuwa ipo katika kipindi cha mpito kuelekea katika mafanikio yatakayowashangaza wengi.

Kutokana na imani yake hiyo, ameshauri ni vyema wakatoa ushirikiano wa kila aina kwa viongozi, wachezaji na benchi lote la ufundi, vivyo hivyo akiwataka viongozi kushikamana na wachezaji na benchi la ufundi, badala ya kuanza kunyoosheana vidole.

Aliyasema hayo mapema leo alipokuwa anazungumzia mwenendo wa klabu hiyo aliyowahi kuifadhili na kuipa mafanikio makubwa katika miaka ya 1990, lakini msimu huu ukionekana kuyumba, kwani tangu kuanza kwa ligi, imetoka sare katika mecho zake zote sita, hali inayowasonesha `wanazi’ wa klabu hiyo.

Alisema Simba inapitia mapito kama ya Manchester United ya England ambayo tangu kuondoka kwa kocha wake wa zaidi ya robo karne, Sir Alex Ferguson iliyumba na hata kutemeshwa ubingwa kwa aibu, lakini sasa imeanza kurejesha makali.

“Sasa ukiangalia hata Simba si timu mbaya ndiyo maana ingawa haijashinda, haijapoteza mchezo pia. Haya yanatokana na mabadiliko mengi kwa wakati mmoja, kuanzia safu ya uongozi, benchi la ufundi na hata wachezaji…hawa watu wanahitaji kupewa muda. Nakuhakikishia Simba hii itakuwa tishio.

“Lakini wakati nikiwasihi wanachama na wapenzi kuwaunga mkono viongozi, wachezaji na kocha, naamini viongozi nao watumie busara ya kufanya kila linalowezekana kuwafanya wachezaji na makocha kujiamini na kujiona wana deni, lakini si kutishiana kila kukicha.

“Hii si sahihi na kwa mazingira ya vitisho, siku zote watabaki kuwa watu wa wasiwasi na kushindwa kuisaidia timu…tuwape nafasi, hakika mapinduzi ya kisoka yataonekana kwa sababu nimeona timu ina wachezaji wengi wenye vipaji,” alisisitiza Dewji.

Katika msimu huu wa ligi, Simba ilianza ligi kwa kutoka sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga kabla ya kupata sare mbili za matokeo ya 1-1 mbele ya Polisi Moro na Wakuja katika ligi hiyo, Stand United ya Shinyanga. Haikufungana na Yanga iliyokuwa inaaminika ni mara zaidi tangu ilipomnasa kocha Mbrazil Marcio Maximo katikati ya mwaka huu, ikatoka pia sare ya 1-1 na Prisons ya Mbeya na pia na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...