Na Lucas Mboje; Bagamoyo
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja amepongezwa na Wadau mbalimbali nchini kwa kufanikisha kuandaa na kukamilisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Magereza ambapo Wadau kutoka nje ya Jeshi la Magereza wamepata fursa ya kujadili kwa siku mbili Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Pongezi hizo wamezitoa kwa nyakati tofauti mjini Bagamoyo katika Mkutano wa siku mbili wa Wadau wa kupokea maoni juu ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Magereza uliofunguliwa rasmi na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulawakil Novemba 04, 2014 katika Hoteli ya Livingstone - Bagamoyo.
"Tunampongeza sana Kamishna Jenerali Minja hususani kwa kufanikisha rasimu hiyo na tunaamini kutokana na kasi yake ya Utendaji wa kazi rasimu hiyo itawasilishwa mapema Serikali kwa hatua za mwisho," Walisikika wakisema.
Aidha, wameongeza kuwa kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Magereza kutaleta ufanisi katika utendaji na uboreshaji huduma mbalimbali zitolewazo ndani ya Jeshi la hilo.
Awali akitoa maelezo mafupi katika ufunguzi wa Mkutano huo wa Wadau wa kupokea maoni ya Sera ya Taifa ya Magereza, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, John Casmir Minja alisema kuwa chimbuko la kuwa na Sera hiyo ni kubadili utaratibu wa kuwafunga wahalifu magerezani ambao ulianza wakati wa Ukoloni na ulilenga zaidi kuwakomoa na kuwaadabisha.
Jenerali Minja aliongeza kuwa utaratibu huo ulilenga kuwaweka wahalifu kwenye Ulinzi mkali na kuwafanyisha kazi ngumu zisizo na tija nazisizozingatia haki za Binadamu.
Alisema kuwa baada ya Uhuru mwaka 1961, Falsafa ya Magereza ilibadilika kutoka ile ya kukomoa na kuwaadabisha wahalifu na kuwa Urekebishaji na kuzingatia haki za Binadamu.
"Mabadiliko ya kifalsafa pamoja na kuridhiwa kwa Mikataba mbalimbali ya Kimataifa yanatulazimu kuwa na Sera ambayo ndiyo itakuwa dira ya Utekelezaji wa shughuli za kila siku za Jeshi la Magereza," alisema Jenerali Minja.
Aidha Jenerali Minja, aliongeza kuwa sera hiyo inalenga pia kubadili mitizamo ya jamii kuwa magereza ni mahali pa mateso. "Tunataka Magereza ya sasa ionekane ni chuo cha kubadili tabia za wafungwa ili wamalizapo vifungo vyao wawe ni raia wema katika jamii."
Jeshi la Magereza kupitia Wataalam wake limeandaa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Magereza kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Haji Semboja ambapo tayari wadau wote wa ndani na nje ya Jeshi la Magereza wamepata fursa ya kuchangia maoni yao kikamilifu tayari kuwasilishwa rasmi Serikalini kwa hatua za mwisho
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulawakil akitoa hotuba ya Ufungaji wa Mkutano wa Wadau uliohusu upokeaji wa maoni ya Sera ya Taifa ya Magereza. Mkutano huo wa siku mbili umefanyikia katika Hoteli ya Livingstone Bagamoyo ambapo wadau wamepitia rasimu hiyo na kutoa maoni kikamilifu Novemba 05, 2014.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulawakil kutoa hotuba ya Ufungaji wa Mkutano wa Wadau uliohusu upokeaji wa maoni ya Sera ya Taifa ya Magereza.
Mchumi kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Deonesia Mjema akichangia maoni katika rasimu ya Sera ya Taifa ya Magereza kabla ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulawakil kutoa hotuba ya Ufungaji wa Mkutano wa Wadau uliohusu upokeaji wa maoni ya Sera ya Taifa ya Magereza.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(katikati) akipitia makabrasha wakati wa majadiliano ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Magereza(kulia) ni Mkurugenzi Idara ya Malalamiko Wizara ya Mambo ya Ndani, Bw. A. Shio(kushoto) ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulawaki.
Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma malewa akitolea ufafanuzi wa Haki za Wafungwa wanazostahili kupatiwa wawapo Magerezani wakati wa majadiliano Sera ya Taifa ya Magereza Novemba 05, 2014 katika Hoteli ya Livingstone Bagamoyo.
Wadau wakifuatilia kwa makini hotuba ya ufungaji wa Mkutano wa Wadau uliohusu upokeaji wa maoni ya Sera ya Taifa ya Magereza Novemba 05, 2014 katika Hoteli ya Livingstone Bagamoyo.(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...