Mtaalam Mwelekezi kutoka Kampuni ya Petrogas Bw. Tom Mitro (kushoto) akielekeza namna ya kuandaa mapendekezo ya miradi ( project proposals) mbele ya washiriki wa mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinawasilishwa na Bw. Tim Mitro kutoka kampuni ya Petrogas (hayupo pichani).
Mtaalam Mwelekezi kutoka Kampuni ya Petrogas Bw. Tom Mitro akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo.

Na Greyson Mwase, Bagamoyo

Wataalamu wa Nishati na Madini wametakiwa kushirikisha jamii inayozunguka miradi inayoanzishwa ili kuzuia migogoro inayoweza kutokea kutokana na wananchi kukosa uelewa na miradi mipya.

Wito huo umetolewa na mtaalamu kutoka kampuni ya Petrogas Bw. Tom Mitro katika mafunzo ya jinsi ya kuandaa mapendekezo ya miradi, sera pamoja na utekelezaji wake yanayoendelea mjini Bagamoyo. Mafunzo hayo yalishirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TDGC).

Bw. Mitro alisema kuwa katika nchi nyingi za Afrika hususan zenye rasilimali nyingi kumekuwepo na migogoro mikubwa katika uanzishwaji wa miradi kutokana na jamii kutoshirikishwa kabla ya kuanzishwa kwa miradi.

Alisema katika hatua za awali za maandalizi ya miradi, wadau mbalimbali muhimu wamekuwa wakishirikishwa ikiwa ni pamoja na taasisi za kifedha, serikali, wanasiasa, wahisani huku kundi la jamii inayozunguka miradi husika likisahauliwa kabisa.

Akielezea athari za kutowashirikisha jamii inayozunguka miradi Bw. Mitro alisema kuwa ni pamoja na migogoro inayopelekea kukwama kwa miradi hali inayopelekea miradi kutokamilika kwa wakati.

“ Wananchi wengi wanapokosa uelewa wa miradi yenye manufaa kwa taifa, matokeo yake ni kuipinga hali inayopelekea kukwama kwa miradi hiyo.” Alisema Bw. Mitro. Bw. Mitro alisema kuwa jamii inayozunguka miradi pamoja na asasi za kiraia zina umuhimu mkubwa sana katika ushirikishwaji katika uanzishaji wa miradi kwani ndio walinzi wa miradi husika hususan miundombinu yake.

Akilelezea jinsi jamii inayozunguka miradi inavyoweza kushirikishwa Bw. Mitro alieleza kuwa ni pamoja na mikutano ya mara kwa mara na wananchi ikiwa ni pamoja na wawakilishi wao na kusisitiza kuwa wanaposhirikishwa katika kila hatua ya mradi wanakuwa mabalozi kwa wananchi wenzao.

Aliongeza kuwa ushirikishwaji wa jamii unaifanya jamii kuwa sehemu ya umiliki wa miradi na kulinda miundombinu yake.

Mafunzo hayo yameandaliwa na mradi unaohusika na kuwajengea uwezo wataalamu wa nishati na tasnia ya uziduaji (CADESE; Capacity Development in the Energy Sector & Extractive Industries) lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wataalamu kutoka sekta za nishati na madini katika uandaaji wa mapendekezo ya miradi mbalimbali ( project proposals) na sera na hivyo kuepusha gharama ya kutumia wataalamu kutoka nje na kukuza umiliki.

Mafunzo hayo yatakayochukua wiki tatu yatashirikisha washiriki 60 ambapo kila kundi la washiriki 20 litajifunza kwa muda wa wiki moja. Kundi la kwanza litajifunza juu ya uandaaji wa mapendekezo ya miradi na kufanya tathmini yake ( project proposals preparations and evaluations ), kundi la pili litajifunza juu ya uandaaji wa sera na kundi la tatu litajifunza juu ya usimamizi wa miradi.

Mradi wa CADESE unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Maendeleo (UNDP) ulianzishwa mwaka huu unatekelezwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Uogozi na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...